20 January 2012

Serikali, madaktari, wafikishana pabaya

Na Rehemu Maigala

MVUTANO kati ya madaktari na Serikali, sasa umechukua sura mpya na kuonekana sawa na mchezo wa kuigiza
baada ya pande hizo kushindwa kukutana jana kila upande ukidai kukodi ukumbi wa kukutana ili kutafuta suluhisho la mgogoro huo.
Dalili za pande hizo kutoaminiana, zilianza kujionesha juzi na ndicho kilichotokea jana baada ya madaktari kukodi ukumbi wa Don Bosco na kukaa kwenye viti wakimsubiri Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Lucy Nkya.
Ilipofika saa sita mchana, madaktari hao walipigiwa simu na kujulishwa kuwa, wanapaswa kuhudhuria mkutano huo katika ukumbi wa Anatoglou, Mnazi mmoja.
Wakati simu hiyo ikipigwa, tayari Dkt. Nkya alikuwa amefika ukumbini na kuagiza madaktari hao, wawe wamefika ukumbini hapo baada ya nusu saa lakini ilishindikana kwa sababu wengi wao walikuwa hawajafika katika ukumbi wa Don Bosco, hivyo waliendelea kusubiriana.
Baada ya madaktari hao kutimia, walikataa kwenda Anatoglou kuonana na Dkt. Nkya kwa madai kuwa, wao ndio wenyeji wake hivyo alitakiwa kuwafuata.
Waandishi wa habari waliokuwepo eneo hilo, walienda Anatoglou na kukuta Dkt. Nkya akiwasubiri madaktari.
Viti kama mnavyoviona hakuna daktari aliyefika ili niwasikilize,  kuanzia leo, sitaki vikao viendelee, waendelee na kazi kama kawaida,¡± alisema na kuongeza kuwa, zikifika siku saba kama madaktari wataendelea na vikao hivyo, watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema wenye malalamiko wayapeleke kwenye Chama wa Wafanyakazi wa Sekta ya Afya na Serikali Kuu (TUGHE) ili wasikilizwe.
Kwa upande wao, madaktari hao walisema msimamo wao upo pale pale na vikao vitaendelea hadi Serikali itakaposikiliza hoja zao.
Akizungumza kwa niaba yao, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, (MAT), Dkt. Namana Mkopi, alisema vikao hivyo vitaendedelea leo kwani hakuna kiongozi hata mmoja katika Wizara hiyo ambaye yupo tayari kuwasikiliza.
Kutokana na hali hiyo, madaktari hao walitoa hoja ya kutaka kuonana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda,  ili asikilize kilio chao.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata, zinasema tayari madaktari kutoka mikoani wamewasili Dar es Salaam kuwaunga mkono wenzao ili kushinikiza madai yao.

No comments:

Post a Comment