19 January 2012

KINAPA watangaza vita kwa majangili

Na Florah Temba, Kilimanjaro

HIFADHI ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) inakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo kuendelea kuwepo kwa matukio ya ujangili hususani ya ukataji wa miti ya asili kwa matumizi ya fito, kuni, nguzo, mbao na uchomaji moto katika misitu ya hifadhi.Hayo yalibainishwa na Mhifadhi Mkuu katika hifadhi hiyo, Bw. Nyamakumbati Mafuru wakati akitoa taarifa ya hifadhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Leonidas Gama aliyekuwa na ziara ya siku moja ya kutembelea hifadhi hiyo kwa lengo la kujionea hali halisi ya utendaji kazi hivi karibuni.
Bw.Mafuru alisema, tatizo sugu linalowasumbua ni upasuaji haramu wa mbao maeneo ya msitu wa asili yanayopakana na vijiji vya Kibosho, Sungu, Uru, Njari, Uru shimbwe, Kieri, Nkweshoo, Kilema na Kishisha.
Alisema, changamoto nyingine inayowakabili ni ulishaji wa mifugo katika hifadhi kinyume cha sheria pamoja na uwindaji haramu wa wanyama katika hifadhi.
“Matukio ya ujangili ya uharibifu ambayo yamekuwa yakijitokeza ni pamoja na uwindaji haramu wa wanyama, uvunaji haramu wa miti yaani ukataji wa fito, kuni, nguzo na upasuaji mbao, ulishaji haramu wa mifugo na uchomaji moto,” alisema Bw. Mafuru.
Katika kukabiliana na uhalifu huo hasa uvunaji haramu wa maliasili na ulishaji mifugo, Bw.Mafuru alisema, wanaendeleza doria maeneo mbalimbali ya mlima hasa katika msitu wa asili.
Alisema, katika kipindi cha miezi sita iliyopita hifadhi ilikamata jumla ya majangili 199 ndani, na baadhi nje ya hifadhi wakiwa na jumla ya mbao 239, nguzo 144 za miti ya asili, ng'ombe 46, mbuzi 50, misumeno 31, mapanga 19, mashoka 25, kamba za manila 87 na pikipiki moja.
Alisema, majangili hao walifikishwa katika mahakama za wilaya zinazozunguka hifadhi ambapo jumla ya kesi 110 zilifunguliwa na kesi 44 zilimalizika na majangili 33 walifungwa kifungo cha kuanzia miezi sita hadi miaka miwili  huku 11 wakitozwa faini.
Mbali na hayo alisema, wamiliki wa ng'ombe na mbuzi waliokamatwa ndani ya hifadhi walitozwa faini ya sh. milioni 1,250,000 ikiwa ni njia moja wapo ya kudhibiti ulishaji mifugo ndani ya hifadhi.
Kwa upande wake, Bw. Leonidas Gama aliupongeza uongozi wa hifadhi hiyo kwa juhudi mbalimbali walizonazo katika kulinda hifadhi na kuwataka kuweka mpango mkakati wa kudhibiti uhribifu katika mlima Kilimanjaro ikiwemo matukio ya ujangili na uchomaji moto.

No comments:

Post a Comment