26 January 2012

AZAM FC YAINYWESHA AFRICAN LYON 2-1

Na Speciroza Joseph

TIMU ya Azam FC, jana ilitoka kifua mbele katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa African Lyon, mabao 2-1 iliyopigwa Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya Dar es Salaam.



Kwa matokeo hayo Azam imepanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na pointi 26, sawa na JKT Oljoro isipokuwa zimetofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika msimao wa ligi hiyo, Simba inaongoza kwa kuwa na pointi 31 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 28.

Azama ndiyo iliyoanza kupata bao dakika ya 16, baada ya beki wa African Lyon kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa shuti la Agrey Morris.

Baada ya bao hilo, African Lyon ilikuja juu na kusawazisha dakika ya 21 kupitia kwa Semmy Kesi, kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Azam FC, Mwadini Ally.

Dakika ya 36, John Bocco aliipatia Azam bao la pili baada ya kuunganisha mpira wa kona iliyochongwa na Abdi Kassim 'Babi'.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza kwa nguvu, huku kila moja ikijaribu kutafuta mabao, lakini mabeki wa pande zote walikuwa imara kuondoa hatari.

Azam iliwatoa Bocco, Jabir Azzi na Kipre Tchetche na nafasi zao kuchukuliwa na Gaudence Mwaikimba, Ibrahim Mwaipopo na Abdulhalim Humud.

African Lyon nayo iliwatoa, Hood Mayanga na Justine Anene na kuwaingiza Idd Mbaga na Hamis Thabit. 

Mabadiliko hayo yaliiongezea kasi, African Lyon ambayo ilikuja juu na kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa wapinzani wao lakini mshambuliaji wake, Sino Agustino dakika ya 87 alishindwa kufunga baada ya kupiga mpira nje akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.

Dakika ya 89, African Lyon ilifanya shambulizi lingine la nguvu lakini Razak Khalfan, aliachia shuti kali lililodakwa na kipa wa Azam.

No comments:

Post a Comment