28 December 2011

Hamad Rashid aikataa kamati

*Asema wajumbe wake hawana sifa, akataa kuhojiwa
*Ataka ufafanuzi katiba iliyoruhusu kamati kumuhoji
*Tuhuma zake sasa kufikishwa kwenye Kamati Kuu


Na Agnes Mwaijega

MBUNGE wa Wawi, Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohammed, jana aligoma kuhojiwa na
Kamati ya Nidhamu na Maadili ya Chama cha Wananchi (CUF), akidai kuwa wajumbe watano kati ya nane ambao wanaunda kamati hiyo, hawana sifa zinazostahili.

Bw. Mohammed aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuitwa na kamati hiyo ili iweze kumuhoji juu ya tuhuma mbalimbali alizozitoa hivi karibuni kupitia vyombo vya habari.

Alisema utaratibu uliotumika kuwateua wajumbe hao, haukuzingatia kanuni na taratibu hivyo hakuwa tayari kuhojiwa na kamati hiyo ambayo imeamua kupeleka suala hilo katika Kikao cha Baraza Kuu.

“Mimi binafsi sina tatizo na suala langu kupelekwa kwenye Kikao cha Baraza Kuu, nipo tayari kwenda kuhojiwa nikiitwa ili niweze kujibu tuhuma za kukiuka utaratibu na katiba ya chama,” alisema.

Aliongeza kuwa, migongano inayoendelea ndani ya CUF, inatokana na majungu yaliyokithiri ndani ya chama hicho hivyo ni wazi kwamba hakifanyi kazi kama taasisi.

“Mimi siogopi kufukuzwa uanachama, hata nikiondolewa jukumu langu la kuhudumia wapiga kura wangu litapaki pale pale, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, anapaswa kujiuzulu nafasi hii kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kuvunja kanuni na sheria za chama,” alisema.

Bw. Mohammed alisema, Bw. Hamad hakupaswa kushauri yeye na wajumbe wengine wa chama hicho wafukuzwe kwa sababu zisizo za msingi ambazo zinalenga kuua nguvu ya watu wenye malengo ya kuhakikisha chama hicho kinapata maendeleo.

“Binafsi nashangazwa na utaratibu unaofanywa na viongozi wa CUF, wamekuwa wakifanya maamuzi na mipango mbalimbali bila kushirikisha wananchama, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alishafanya maamuzi ya kuonesha watu wanaotakiwa kufukuzwa ndani ya chama nikiwemo mimi na wenzangu.

“Maamuzi haya aliyatuma kwa njia ya mtandao kwenda kwa Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, ujumbe huo tuliukamata mimi na wenzangu na nyaraka tunazo,” alisema.

Aliongeza kuwa, hadi sasa haelewi anatuhumiwa kwa lipi kwani kila kukicha, tuhuma dhidi yake zimekuwa zikibadilika kwani kuna maneno mengi yaanayozungumzwa dhidi yake kila siku kwa lengo la kumchafua na kumuondolea sifa katika jamii.

“Mimi sishangazwi sana na tuhuma hizi ambazo hazi na hoja za msingi, suala la mimi na baadhi ya wajumbe kufukuzwa uanachama liliandaliwa muda mrefu, lilikuwa likisukiwa mpango siku hadi siku kuhakikisha tunaondoka ndani ya chama,” alisema.

Aliongeza kuwa, mfumo wa CUF unamshangaza kwa sababu chama hicho kimeshindwa kutafuta suluhu na wanachama wake ili kufikia muafaka jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya chama hicho.

Alisema chama hicho kipo katika hatari kubwa ya kupoteza sifa yake kwa sababu kina wafuasi ambao wako kwa ajili ya kufanya maandamano na mikutano ya hadhara badala ya kujikita katia  mabadiliko ndani ya chama.

Alitoa wito wanachama wa CUF wenye mapenzi na chama hicho, kuunga mkono juhudi za watu wenye uchungu na maendeleo ya chama hicho.

Taarifa ambazo Majira ilizipata kutoka ndani ya kikao ambacho Bw. Mohammed alikipinga na kukataa kuhojiwa, zilisema kabla kikao hicho hakijaanza, mbunge huyo aliibua hoja iliyowataka wajumbe kumweleza katiba iliyowaruhusu kuendesha kikao hicho.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Bw. Hamisi Machano, alimjibu Bw. Mohammed kuwa katiba inayotumika ni cham hicho.

Pamoja na kupewa jibu hilo, aliuliza swali lingine kuwa, katiba hiyo ni ya toleo gani na kujibiwa kuwa ni ya toleo la mwaka 2003.

Baada ya majibu hayo, Bw. Mohammed alikieleza kikao hicho kuwa, hakubaliani na baadhi ya wajumbe waliochaguliwa kumuhoji.

Wajumbe alioonesha kuwa na wasiwasi nao ni Mwenyekiti Bw. Machano, Katibu wa kamati Bw. Hamisi Hasani, Bw. Kambaya na Bw. Riziki Juma ambaye ni mbunge.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, Bw. Mohammed aliwataka wajumbe hao wampe tuhuma zinazomkabili jambo ambalo lilipingwa na wajumbe kwa maelezo kuwa, si sahihi kumpa tuhuma mjumbe ambaye hakubaliani na wajumbe wa kamati hiyo.

Baada ya kushindwa kuelewana na wajumbe, walianza mabishano ambapo Bw. Mohammed alisema ni haki ya mwanchama kusomewa tuhuma zake jambo ambalo lilipingwa na wajumbe wa kamati.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Mohammed alisema ni haki ya kila Mtanzania kupata taarifa kwa mujibu ya Katiba ya nchi lakini wajumbe hao walisema, Katiba inayotumika katika kikao hicho ni ya chama na si nchi.

Bw. Mohammed alizidi kuwaambia wajumbe hao kuwa, hata mahakamani mahakamani mtuhumiwa anaweza kumkataa hakimu, akajibiwa kuwa hata mtuhumiwa akikataa hakimu atabadilishiwa na sio kufutwa kwa mashtaka.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu, Bw. Kambaya, alisema msimamo wa Bw. Mohammed hautaizuia kamati hiyo kuendelea na taratibu zake kwani inafanya kazi kwa kuzingatia katiba ya chama.

6 comments:

  1. Malizaneni tu, kwani kama mnataka kummwaga mpaka mzunguke kote huko: fanyeni kama nccr mageuzi. Tumewachoka kila siku ninyi tu, kama siyo CUF ni CHADEMA ingawa sasa wamepoa kidogo wapo likizo wakiibuka huko Watanzania kuweni tayari. Mtaona mambo yanavyoripuka, lakini bilashaka usalama wa taifa wamekwisha yapata hayo matarisho kazi kwao: Watanzania Tufanye kazi ili tujiletee maendeleo tuachane na Porojo za hawa jamaaa.

    ReplyDelete
  2. Uliyetoa maoni hapo juu inabidi uende shule:kwa taaarifa yako maendeleo bila siasa bora huwezi kujitenga na siasa utakuwa umejimaliza.
    rejea elimu ya siasa ndogo tu iliyofundishwa shule ya msingi ili tuendelee tunahitaji siasa safi,uongozi bora, ardhi na watu. tunahitaji vyama imara vyenye uwezo wa kuchukua hatua pale mtu anapokosea ,hatuhitaji vyama vya kubebana, hatuhitaji vyama vyenye watu wasioweza kuguswa kwa kuwa tu wao wana vyeo.vyama kuweni imara ondoeni mamruki wote bila kuogopa;wote waliopandikizwa na usalama wa taifa uliopo kwa niba ya CCM Waondoeni msiogope kusemwa na haohao wanaotaka malengo yao yatimie. chadama kaza buti na wengine wote kazeni buti CCM wanahaha.

    ReplyDelete
  3. Nd. Hamad Rashd tulikuwa tunakupa heshma kubwa kama kiongozi mwenye upeo na anayeweza kuongoza moja katika nchi hii, kumbe vile unauchu wa madaraka na fedha. hv viruzuku vinavyopatika vnakutoeni roho, kwani nani kwakwambieni lazima muwe viongozi, hapo ulipata huko bungeni pashatosha, tushakuona hufaii. ayo maneno yako hubu njoo useme huku jimboni kwako uone kama hutopigwa mawe. kiongozi kama wewe hufai na tushafukuza wengi kama wewe wanaopenda madaraka na fedha. unapenda uluwa, unajikweza unafikiri sisi sote wwajinga wewe ndo mwenyeakili, tulikupa heshma lakini ushaipoteza. Huku zanzibar usije hatukutaki. mara hii anzisha chama chako wewe na waroho wenzio. huna maadili sio mwerevu, kama unataka uongozi sisi ndio tunaekupa sio wewe.

    ReplyDelete
  4. Hapa tatizo si Hamad bali Seif na uroho wake wa madaraka. Ameamua kuwasaliti CUF na kujiingiza kwenye kuwa nyumba ndogo ya CCM bila hata aibu. Angalia hata makamu wa pili wa rais wa Zanzibar anavyopata coverage kubwa kwenye vyombo vya habari kuliko huyu kimada wa CCM ambaye yupo kama kibonzo ofisini akifanya kazi zisizojulikana wala kuwepo. Shame on you Shariff!

    ReplyDelete
  5. Mchawi pekee ni Maalim, na asipoangaliwa kwa makini hata muungano atauvunja huyo maadam sasa hakuna mtu mwenye sauti ya kusikilizwa na kuaminiwa na wananchi. Hamad Seif ni kati ya wanasiasa hatari kubwa. Hawaoni taabu kuwatumia wananchi hadi kupoteza maisha ari mradi tu wafanikiwe katika malengo yao binafsi. Sasa kapata huo umakamu wa kwanza, muda si mrefu nao utakuwa haumtoshi ataanza kudai zaidi. Matokeo yake yatakuwa ni kuvunja muungano.

    ReplyDelete
  6. wote wale wale fikra mbovu zisizo taka mabadiliko huwa na visingizio, na mtu kama umeona kasoro kwenye nyumba yako kaa na wanafamilia mzungumze yaishe haina haja ya kulaumiana mitaani, Hamad Rashid na Seif yamalizeni matatizo yenu chamani. na vyama vingine angalieni kasoro zenu, kiukweli vyama vyetu hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla vinaongozwa na watu wachache tena kikundi kidogo cha watu ambao wanapoona wanataka kutolewa wanaweka vikwazo na kuwafukuza watu wanaotaka mabadiliko ya kweli katika mifumo ya vyama vyao, hili si kwa CCM pekee yake bali hata upande wa pili wa shilingi vyama vya upizani navyo viko hivyo. Watanzania tufanye kazi tulijenge taifa bila kuangalia wewe ni dini gani? kabila gani? chama gani? na unatoka wapi?

    ReplyDelete