Na Mwandishi Wetu, Mvomero
MKURUGENZI wa Mafunzo na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro Bw. Songa Mgweno, ambaye anayetuhumiwa
kumchoma kisu Diwani wa chama hicho, Kata ya Mtibwa, Bi. Tusekile Mwakyoma, jana amejisalimisha katika Kituo cha Polisi Turiani.
Bw. Mgweno ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho (BAVICHA), alijisalimisha akiwa amevaa sandarusi (mifuko ya plastiki), na kuomba apewe nguo.
Mpelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani hapa, Bw. Hamis Selemani amethibitisha kukamatwa kwa Bw. Mgweno ambaye leo atasafirishwa hadi mkoani chini ya ulinzi mkali.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao walifika kituoni hapo kumuona Bw. Mgweno, walisema kitendo kilichofanywa na kiongozi huyo kimeharibu sifa ya chama wilayani humo.
Mjumbe wa Baraza la Wazee la CHADEMA wilayani humo, Bw. Haji Ngoye alisema, pamoja na Bw. Mgweno kujisalimisha polisi, hakiwezi kumfutia dola katika jamii kutokana na unyama aliofanya kwa kiongozi mwenye dhamana ya kuhudumia wananchi.
“Kitendo hiki kimeharibu sifa ya chama chetu, siwezi kumuwekea dhamana mtu aliyedhamiria kupoteza uhai wa mwenzake, jambo la msingi sheria inapaswa kuchukua mkondo wake,” alisema Bw. Ngoye.
Katibu wa CHADEMA wilayani humo, Bw. Dismas Ngeresha, alisema Kamati ya Utendaji imekutana jana mchana kujadili tukio hilo la kutisha.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum wilayani humo Bi. Juliana Petrol, alilaani kitendo kilichofanywa na Bw. Mgweno ambaye hakupaswa kufanya kitendo cha kikatili kama hicho kutokana na dhamana aliyonayo kama kiongozi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Misheni Bwagala ambako amelazwa diwani huyo, Dkt. Alphonce Mhando, alipoulizwa kuhusu maendeleo ya Bi. Mwakyoma alisema, hawezi kuzungumza na waandishi kwani muda huo alikuwa katika chumba cha upasuaji.
Mwandishi wetu alipokwenda wodi namba 36 alipolazwa diwani huyo, alimkuta Bi. Mwakyoma akiwa ametundikiwa chupa ya damu.
Bw. Mgweno anadaiwa kumchoma kisu Bi. Mwakyoma chini ya ziwa la kushoto na kukimbia usiku wa kuamkia juzi.
No comments:
Post a Comment