28 November 2011

Wanasiasa wanataka kumwaga damu -Mchungaji

*Ataka majadiliano si maandamano Katiba Mpya

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

MWENYEKITI wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini, Mchungaji  Clement Mwaitebele, ameibuka na kukemea
wanasiasa nchini kuwa wana ajenda ya siri kutaka kuleta machafuko na umwagaji wa damu nchini kwa kisingizio cha kudai haki kwa njia ya maandamano na matamshi ya vitisho.

Akitoa tamko la Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) wakati wa Ibada maalumu ya kuzindua Idara ya Umoja wa Wanawake na watoto wa Kanisa hilo jana, Mchungaji Mwaitebele alisema Kanisa kamwe haliwezi kukaa kimya na kubabaishwa na kauli za wanasiasa zinazolenga kuwatisha watanzania.

Alisema kauli za wanasiasa hivi sasa ni za hatari na kuonya kuwa kama kutatoa machafuko nchini watakaokuwa wamesababisha ni wanasiasa ambao ndio wamekuwa wakiwahamasisha watanzania kuchukia amani na utulivu vilivyopo kwa kisingizio cha kudai haki na Katiba Mpya.

Mchungaji Mwaitebele aliyekuwa anazungumza kabla ya kuzindua idara hiyo alisema watanzania wamechoshwa na vitisho vinavyotolewa na wanasiasa kila kukicha na kwamba wenye mustakabali ya amani ya Tanzania ni watanzania ambao ndio wenye utaifa na si wanasiasa na viongozi.

"Nasema tumechoka kuwasikia wanasiasa kwa vitisho vyenu, najua hata sasa mnanisikia acheni kuwatisha watanzania na kuwaona kama hawana haki ya nchi hii, nasema wanayo haki ni mali yao na wao ndio wenye mamlaka ya kujiamulia mambo yao na si wanasiasa ambao mmekuwa mkitoa matamko ambayo ni kwa maslahi yenu," alisema.

Alisema kutokana na matamko hayo ndio maana watanzania walipiga kura ya
kutotaka vyama vingi wakati wa mchakato wa kuingia kwa mfumo wa vyama vingi nchini lakini Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akatumia hekima kwa kuwashauri watanzania kukubali mfumo huo ambao sasa alidai umekuwa ukipelekea matamko ya vitishgo kwa watanzania.

Mchungaji Mwaitebele alisema kuwa kumekuwepo na madai ya katiba ambayo alisema kuwa hakuna haja ya vurugu wala maandamano bali kinachotakiwa ni mazungumzo ya amani bila kuwatisha watanzania ambao wana haki ya kukaa kwa utulivu ndani ya nchi yao.

Alisema Kanisa kamwe halitakubali kuona amani na utulivu vinapotezwa na watu wachache nchini ambao ni wanasiasa ambao wamekuwa wakiendesha harakati za kuhakikisha watanzania wanaikimbia nchi na kuona kuwa si mahali patulivu tena na kuwataka wakristo kote nchini kushirikiana kuiombea nchi amani na mchakato wa Katiba Mpya.

Naye Katibu Mkuu wa KMT Mchungaj Comrad Nguvumali, alisema Kanisa limeamua kuzindua idara hiyo kutokana na kutambua umuhimu wake katika jamii ya watanzania katika suala zima la kuombea amani na utulivu kutokana na wingi na ngu ya kina mama.

Alisema waathirika wa kwanza katika vita baada ya amani kupotea ni wanawake na watoto na hivyo kupitia idara hiyo alisema kanisa litaendesha mafunzo juu ya kutunza amani katika familia zote nchini.

Mshauri wa idara hiyo mhadhiri wa chuo kikuu cha Teofili Kisanji Mchungaji Mary Kategile, alisema kinamama wataendelea kupiga vita kila aina ya uharibifu wa amani nchini kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na jamii yenye utulivu na inayopendana.

No comments:

Post a Comment