Na Mwandishi Wetu, Morogoro
BAADHI ya askari wa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, wametangaza vita na waandishi wa habari mkoani humo kwa madai kuwa, vyombo wanavyoandikia vinawatuhumu
kuhusika na mtandao wa majambazi pamoja na kuwalinda wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Uchunguzi uliofanywa na Majira umebaini kuwa, vita hiyo imetangazwa na baadhi ya askari wanaotuhumiwa kuhusika na mtandao huo.
Awali jeshi hilo lilikuwa karibu na wanahabari lakini hivi sasa, limegeuka adui baada ya wanahabari mkoani humo kufichua vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari wake.
Kiongozi mmoja wa Chama cha Wanahabari wa Habari mkoani Morogoro ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alitoa wito kwa wanahabari kuwa makini wanapotekeleza wajibu wao na kuepuka mambo yanayoweza kuvunja sheria za nchi.
“Nawaomba wanahabari wote kufanya kazi zao kwa umakini mkubwa pamoja na kuepuka uvunjifu wa amani kwani baadhi ya askari tayari wameanza vita dhidi yetu,” alisema kiongozi huyo.
Alisema inashangaza askari hao kutangaza vita ya chini chini badala ya kutekeleza wajibu wao kama walivyofanya wanahabari.
“Kazi ya askari ni kukamata mtu yeyote ambaye itabainika amevunja sheria bila kujali itikadi, cheo, ujamaa, undugu, wala urafiki hivyo wanapaswa kutekeleza wajibu wao.
Baadhi ya wanahabari mkoani humo wamesema kuwa, vitisho hivyo haviwezi kuwakatisha tamaa ya kutekeleza wajibu walionao kwa jamii hivyo wataendelea kuandika habari zinazohusu ubadhirifu, tuhuma, maendeleo na kutoa elimu kwa jamii.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi mkoani humo wamelisihi jeshi hilo kuwakatama wahusika wa biashara ya dawa za kulevya ambao walitajwa na mzazi wa mwanafunzi Elizaphan Shadrack (16) anayesoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Morogoro, Bw. Shadrack Gando.
Wakiongea na Majira, wananchi hao waliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamekithiri kwa biashara hiyo kuwa Manzese Kata ya Mafika, Mjipya, Msamvu, Sultan, Sabasaba naKichangani.
“Maeneo yote tuliyoyataja ni sugu katika biashara hii na polisi wanayafahamu lakini hadi sasa hatufahamu kwanini wahusika wa biashara hii hawakamatwi,” walisema.
Waliongeza kuwa, Mkoa huo ni sawa na bandari ndogo ya kusafirisha dawa hizo kwenda mikoa mingine nchini ambapo vijana wengi wameharibikiwa kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Majira lilipomtafuta Kamanda wa Polisi mkoani humo, Adolfina Chialo, ili kuzingumzia vitisho vinavyotolewa na baadhi ya askari wake kwa wanahabari mkoani humo alisema, taarifa hizo hazijamfikia kama kiongozi wa polisi mkoani humo.
Mwisho.
“Jukumu la wanahabari ni kuandika habari ili mradi wanazingatia taratibu na maadili ya kazi zao,” alisema Kamanda Chialo.
No comments:
Post a Comment