Na Esther Macha, Mbeya
WENYEVITI wa NCCR-Mageuzi katika wilaya zote mkoani Mbeya, wamemtaka Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Bw. James Mbatia, kujiuzulu wadhifa wake kwa
madai ya kusababisha chama hicho kikose maendeleo.
Akizungumza na Majira kwa niaba ya wenyeviti hao, Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa, Bw. Robnson Fongo, alisema uamuzi huo umefikiwa na viongozi hao baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa Bw. Mbatia kama kiongozi wa juu katika chama.
Alisema Bw. Mbatia amekuwa akiamua mambo ya chama yeye binafsi badala ya kushirikisha viongozi wenzake ambao anapaswa kukaa nao ili kukijenga chama hicho.
Aliongeza kuwa, kiongozi huyo pia ameshindwa kuwafanya viongozi waliochaguliwa katika vyombo vya maamuzi kupitia chama hicho kuwa na msimamo wa pamoja katika mambo yenye maslahi kwa chama hicho.
Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho Wilaya ya Chunya Bw. Nyawili Kalenda, alisema kauli zinazotolewa na kiongozi huyo mara kwa mara zinachangia kukibomoa chama hicho badala ya kukijenga.
Katika mkutano huo, wenyeviti nane wa wilaya zote walishiriki kutoa maamuzi hayo na kudai kuwa, ruzuku ya chama hicho imekuwa ikiishia Makao Makuu bila kufika mikoani.
Hivi karibuni, viongozi wa chama hicho mkoani Kigoma nao walitangaza kuunga mkono mkakati wa kumng'oa Bw. Mbatia madarakani.
Azimio hilo limefikiwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho mkoani humo katika kikao chao kilichofanyika wilayani Kasulu na kuhusisha wenyeviti wa majimbo manne ya uchaguzi mkoani humo.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe hao walijadili kwa kina changamoto na mafanikio waliyopata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ndipo ikaibuka hoja ya kumkataa Bw. Mbatia kwa madai mwenyekiti huyo hana dhamira ya kweli kukiongoza chama hicho ili kiweze kushika dola.
Walisema Bw. Mbatia amekuwa akitumia ruzuku ya chama kwa maslahi binafsi, kujenga makundi kwa viongozi na wanachama na kutoujali mkoa huo ambao ndiyo wenye wabunge wa chama hicho.
Mjumbe kutoka Jimbo la Kigoma Mjini, Bw. Said Milindi, alisema umefika wakati wa kumshinikiza Bw. Mbatia kuachia madaraka aliyonayo ili kutoa nafasi kwa wanachama kuchagua kiongozi ambaye atakiwezesha chama hicho kupata mafanikio kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa upande wao, wajumbe kutoka Kigoma Kaskazini, Kusini, Muhambwe na Buyungu, walimtuhumu Bw. Mbatia kwa madai kuwa ni mpinzani wa vyama vya upinzani.
“Kitendo hiki si kizuri hata kidogo, kinachangia kuvunja upinzani na kukipa nafasi chama tawala kiendelee kuongoza, umefika wakati wa kumshauri aondoke madarakani ili apishe wengine ambaye atatimiza malengo yetu kama chama cha upinzani,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Kigoma Kusini, Bw. Venance Mwaka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jimbo la Muhambwe, Bw. Alex Mpambayifyisi, aliunga mkono mkakati wa kumng’oa Bw. Mbatia akimtuhumu ameshindwa kutengeneza kadi za wanachama ili kuhamasisha wanachama wapya wajiunge na chama hicho.
Jumla ya wajumbe 12 wakiongozwa na Mwenyekiti wa kikao hicho, Bw. Mahamudu Tungirayokama na waasisi wa chama hicho mkoani humo, walishiriki kikao hicho ambacho kiliazimia Bw. Mbatia aachie wadhifa alionao ili kukinusuru chama hicho.
Majira lilipomtafuta Bw. Mbatia katika simu yake ya mkononi ili aweze kujibu tuhuma hizo, hakupatikana kwa kuwa ilikuwa imezimwa.
Mabatia, Mrema, Cheyo, Dovutwa - siongelei harusi ya CUF - hawa wote si wapinzani bali walamba viatu wanaosubiri Kikwete afurahi na kauli na vitendo vyao vya kusaliti upinzani ili awarushie makombo, hawa ni walamba viatu na wako tayari kulamba hata mahali pabaya ilihali wawafurahishe mabwana wao wa CCM.
ReplyDeleteMbatia amekifanya chama cha NCCR kidorore. Hana mawazo mapya na amedhihirisha umamluki wake katika juhudi tunazoziona kuudhoofisha upinzani. Sioni kwanini asijiengue mwenyewe. Ni mpaka angólewa ajue ameshindwa?
ReplyDelete