29 November 2011

Mtoto auawa akidaiwa kuiba sh. 10,000

*Akatwa mapanga mwili mzima
*Petroli yalipua nyumba, 2 wafa


Na John Gagarini, Kibaha

WATU sita wamekufa mkoani Pwani katika matukio tofauti likiwemo la mtoto Kelvin Mapundu (7), mwanafunzi wa
darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Dondwe, kukatwa mapanga na kuuawa akituhumiwa kuiba sh. 10,000.

Akizungumza na Majira jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Mangu, alisema tukio hilo lilitokea Novemba 26 mwaka huu, saa tano asubuhi katika Kijiji cha Dondwe, wilayani Mkuranga.

Alisema mtoto huyo anadaiwa kuiba fedha za Bw. Paulo Mtitu (18), mkazi wa kijiji hicho ambaye alichukua panga na kumkata marehemu sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi, atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi,” alisema Kamanda Mangu.

Katika tukio la pili, watu wawili wamekufa na mmoja kujeruhiwa baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuwaka moto ulitokana na mafuta ya petroli ambayo yalihifadhiwa ndani ya nyumba hiyo.

Kamanda Mangu alisema, nyumba hiyo ilikuwa imeezekwa kwa nyasi ambapo mmiliki wake, alikuwa akifanya biashara ya kuuza mafuta hayo kwa waendesha pikipiki.

“Tukio hili lilitokea Novemba 26 mwaka huu, saa moja usiku katika eneo la Mbwewe, Wilaya ya Bagamoyo, nyumba iliyoungua ni mali ya Bw. Sijali Juma (35), ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza mafuta haya nyumbani kwake,” alisema.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Inzingilo Maua (20) na mtoto Neema Sijali (4) ambapo mtoto Fatuma Sijali (4), alijeruhiwa.

Kamanda Mangu alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Zahanati ya Mbwewe wakati mtoto Sijali anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha.

Katika tuki jingine Mwenyekiti wa Kitongoji cha Binga, Bw. Salum Kilenya (44) mkazi wa Sotele C, amekufa baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni.

Kamanda Mangu alisema, tukio hilo lilitokea Novemba 27 mwaaka huu, saa sita usiku katika Kijiji cha Sotele, wialani Mkuranga.

“Hadi sasa mtu anayetuhimiwa kufanya mauaji haya ni Bw. Jacob Benard (43) ambaye ni fundi ujenzi wa Bunju B, chanzo cha mauaji wivu wa mapenzi, walikuwa wakigombea mwanamke,” alisema.

Aliongeza kuwa, jeshi hilo linawashikilia watu wanne kuhusiana na mauaji hayo.

Wakati huo huo, Kamanda Mangu alisema, mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Martin Geibner (48) raia wa  Ujerumani amekufa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga gari lingine.

Tukio hilo limetokea Novemba 27 mwaka huu, saa 10 jioni, katika eneo la Bonde la Mkaramo Mlandizi, wilayani Kibaha, barabara ya Dar es Salaam-Morogoro.

Alisema  Bw. Geibner alikuwa akiendesha gari yenye namba za usajili T 116 ANS aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro ambalo liligonga lori aina ya Tata Tipa, yenye namba T 699 BBT.

“Magari haya yaligongana uso kwa uso, abiria waliokuwa katika gari ndogo walijeruhiwa ambao ni Ingrid Geibner (44), Leo Geibner (9) na Yonas Geibner, wote wakazi wa Morogoro Junior Seminary, ambao wote wamelazwa Hospitali ya Tumbi,” alisema Kamanda Mangu.

Aliongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi gari aliyokuwa ikiendeshwa na marehemu ambaye alikuwa akiyapita magari mengine katika eneo ambalo si salama.

No comments:

Post a Comment