25 October 2011

Polisi 8 mbaroni wizi wa stika makao makuu ya Trafic

Na Stella Aron

JESHI la Polisi limewatia nguvuni askari wake wanane kwa kuhusika na wizi wa stika za wiki ya nenda kwa usalama zilizoibiwa hivi
karibuni katika Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarabi Kamanda Mohamed Mpinga, Makao Makuu ya kikosi hicho Jijini Dar es Salaam.

zinazodaiwa kufikia zaidi ya milioni 16.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam jana, Kamanda Mpinga alisema kikosi chake kimesikitishwa na wizi huo ambao umesababisha hasara kubwa kutokana na tamaa za watu wachache.

"Hadi sasa tunawashikilia askari nane kwa ajili ya mahojiano lakini kati ya hao tayari askari wawili tumewabaini kuhusika moja kwa moja na tukio hilo ambapo watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka, " alisema Kamanda Mpinga.

Akitoa ufafanui wa kina alisema stika zilizoibiwa ni 4500 ambapo kati ya hizo 3000 ni za magari madogo na 1500 ni za magari makubwa. Kwa mahesabu ya harakaharaka zinakadiriwa kufika sh.milioni 16.

Alisema katika kuhakikisha kuwa stika hizo hazizagai mitaani kwa ajili ya kuuzwa tayari wamesambazwa namba za stika zilizoibiwa nchi nzima.

Alizitaja mabunda ya namba za stika yaliyobiwa kwa magari madogo kuwa ni 0049001-0049500, 0050501- 0051000, 0052001-0052500, 0052501-0053000, 0053001- 0053500 na 0053001- 0053500.

Kwa upande wa magari makubwa mabunda yaliyobiwa ni yenye namba zinazoanzia 0176501- 0177000, 0179501- 0180000 na 0154001-0154500

Kamanda Mpinga alisema jeshi hilo linatoa onyo kwa wananchi kuwa makini na namba hizo na kuomba yeyote atakayebaini kuuziwa stika zenye namba hizo atoe taarifa haraka katika kituo chochote cha polisi ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua.

"Tunatoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na namba hizo na yeyote atakayebaini kuuziwa stika zenye namba hizo atoe taarifa katika kituo cha polisi na watuhumiwa tutawachukulia hatua haraka," alisema Kamanda Mpinga.

Hata hivyo alisema jeshi hilo bado linaendelea na upelelezi zaidi kuwatambua watuhumiwa wengine na kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa askari wengine wenye tabia hiyo chafu inayotia doa polisi mbele ya jamii.

Akizungumzia kushikiliwa kwa askari hao Kamanda wa Mkoa wa kipolisi Ilala Bw. Faustine Shilogile, alithibitisha kukamatwa kwa askari hao kwa mahojiano zaidi.

Alisema askari hao wanaendelea kuhojiwa wakiwa nje huku upelelezi ukiendelea na mara baada ya kukamilika hatua zingine zitatangazwa.

"Tunaendelea kuwahojia askari wawili hadi sasa kwa ajili ya tukio hilo na baada ya kukamilika tutatoa taarifa zaidi, " alisema kamanda Shilogile.

1 comment:

  1. Kitendo hiki kinadhihilisha kuporomoka kwa kwa maadili ndani ya Jeshi la Polisi

    ReplyDelete