26 October 2011

Kibadeni aenda kuhiji Makkah

Na Mwandishi Wetu

MENEJA wa timu ya Simba, Abdallah Kibadeni 'King Mputa,' ameondoka nchini leo kwenda kuhiji Makkah, Saudi Arabia na amewaahidi
wana Simba kuwa, atamwomba Mungu timu hiyo itwae ubingwa wa Tanzania Barana Afrika msimu huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga alisema Meneja huyo anakwenda kuhiji Makkah, ambapo atakuwa huko kwa wiki tatu.

“Kibadeni anaipenda Simba ni timu iliyomlea hadi kufikia hapa alipo ni kwa sababu ya klabu hii. Ni jambo la faraja kwenda kuhiji akitokea Simba. Anapenda kuwashukuru wana Simba wote kwa sababu dua zao na mapenzi yao kwake, ndizo zilizomfikisha hapo.

“Katika safari yake ya hija, zaidi ya mambo mengine atakayoyaombea, ataomba pia kwamba Mungu aijalie Simba ili itwae ubingwa wa Tanzania msimu huu na pia ule wa michuano ya CAF kwa vile anaamini timu nzuri tunayo,” alisema.

Kibadeni ni muumini wa dini ya kiislamu na hija ni mojawapo ya nguzo tano au misingi ya dini hiyo.

Meneja huyo, ambaye pia ni miongoni mwa wachezaji bora wa wakati wote wa Wekundu wa Msimbazi, atakuwa Makkah kwa kipindi cha wiki tatu.

Mchezaji huyo wa zamani, ameondoka wakati wa maandalizi ya pambano la watani wa jadi Jumamosi, ambapo alisema matumaini yake ni makubwa kwa timu yao kuibuka kidedea katika pambano hilo.

Katika kipindi ambacho, Kibadeni hatakuwepo nafasi yake itashikiliwa na nahodha wa zamani wa Simba, Nicholaus Nyagawa.

2 comments:

  1. Nawashangaa wa bongo, King Kibaden yupo na makocha wengine kibao wanaweza kufundisha Simba, Yanga mpaka Taifa Stars lakini tumekazana kuwaajili makocha wageni. Halafu kuna wabongo wako buzy wanawakatalia waTanzania wenzao wa ughaibuni kuwa na uraia pacha,(ambao ni dada na kaka zako) lakini wanawakaribisha wageni kwa mikono mingapu sijui. Tanzania nzima inatawaliwa na wageni, uwekazaji mpaka michezo. Yaani aingii akilini. Tumerudi kwa mkoloni kwa kuwakaribisha wenyewe.

    ReplyDelete
  2. Jamani watu wa Majira. Hili ni gazeti ninalolipenda sana nikiwa Bongo kwa namna linavyotoa taarifa bila kupendelea. Lakini kwa sasa nipo nje ya nchi na nalisoma kupitia mtanda. Sasa cha ajabu ni kwamba limepitwa na wakati sana katika mtandao ukilinganisha na magazeti mengine. Habari zinazopatikana si za leo wala jana bali za zamani sana. ahaebu tupeni habari ambazo ni current jamani

    ReplyDelete