15 August 2011

Bei ya mafuta juu tena

Na Grace Michael

FURAHA ya watumiaji wa mafuta kwa bei bidhaa hiyo kuteremshwa kwa asilimia 9 na kusababisha wafanyabiashara wa mafuta kugoma, ilikuwa ya muda tu na
sasa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupanda tena kwa kati ya asilimia 5 na 6 kuanzia leo.

Bei hizo zilizotangazwa na mamlaka hiyo Dar es Salaam jana na kutanza kutumika leo, zimeongezeka kwa asilimia 5.51 kwa petroli, dizeli (6.30%) na mafuta ya taa 5.30%. Hivyo, petroli itauzwa kwa sh. 100.34 zaidi ya bei elekezi ya iliyoleta kizaazaa wiki iliyopita, dizeli kwa sh. 120.47 zaidi na mafuta ya taa kwa sh. 100.87.

Akitangaza mabadiliko ya bei hizo, Meneja Biashara wa Mazao ya Petroli wa EWURA, Mhandisi Godwin Samwel, alisema kuwa kupanda kwa bei hizo kunatokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani.

Alisema kuwa kwa viwango vya bei vilivyotumika katika chapisho hilo jipya, bei katika soko la dunia zimepanda kwa wastani wa asilimia 5.42 huku thamani ya shilingi ya Tanzania ikishuka kwa shilingi 47.12 ambayo ni sawa na asilimia 296 kwa dola moja ya Marekani.

Bei ya mafuta ya petroli kwa Mkoa wa Dar es Salaam na bei za awali kwenye mabano ni sh. 2,114.12 (sh. 2,004), dizeli 2,031.31 (sh. 1,911) huku mafuta ya taa yakiwa sh. 2,005.40 (sh. 1,905) kwa lita.

Hata hivyo, Mhandisi Samwel alisema kuwa bei hiyo ina unafuu kutokana na kutumika kwa kanuni mpya ya ukokotoaji wa bei, na iwapo ingetumika kanuni ya zamani, petroli kwa Dar es Salaam ineuzwa kwa sh. 2,298.33, dizeli 2,213.36 na mafuta ya taa kwa sh. 2,188.89.

Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko, EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta kwa lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

Aidha alisema kuwa vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za mafuta katika mabango yanayoonekana yakionesha bei, kwa kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vyema kwa wateja.

“Jambo jingine tunalosisitiza ni wanunuzi kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta na bei kwa lita, ili kuwapata wanaouza mafuta kwa bei ambazo hazijapangwa na mamlaka yetu,” alisema.

Hata hivyo EWURA ilisema kuwa bei hizo zinaweza kushuka baadaye endapo hapatakuwa na kupanda zaidi kwa dola ya Marekani au kushuka kwa shilingi ya Tanzania.

Hali ya mafuta

Alisema kuwa hali ya mafuta nchini kwa sasa ni nzuri kwa kuwa mwishoni mwa wiki mafuta yaliuzwa kwa wingi sana vituoni ambapo kwa siku ya Ijumaa jumla ya lita milioni 9.5 ziliuzwa kutoka visima kwenda vituoni na Jumamosi ziliuzwa lita milioni 4.9 na meli zinaendelea kuingia.

Ongezeko hili linakuja siku chache baada ya kumalizika mgogoro uliokuwepo wa wafanyabiashara wa mafuta kugoma kuuza mafuta kutokana na kushuka kwa bei za mafuta hatua iliyosababisha EWURA kuifungia leseni ya kuuza mafuta ya petroli, dizeli na taa Kampuni ya BP kwa muda wa miezi mitatu.

4 comments:

  1. EWURA/SERIKALI INATUFANYA KAMA WATOTO MAANA HATA UAMUZI WA KUPUNGUZA BEI WALIKURUPUKA PIA ILICHUKUWA ZAIDI YA MWEZI BEI MPYA ILIPOANZA KUUZWA TOKEA BUNGE LILIPOPENDEKEZA,SASA LEO BEI JANA TU LEO INAPANDA PIA MAFUTA YALIYOPO NI ZAIDI YA MIEZI 2 IWEJE HAYO YAKUMBWE NA KUPANDA KWA DOLA?MAANA HAYA YALISHANUNULIWA HII NI DANGANYA TOTO,LAKINI IKISHUKA DOLA ITACHUKUWA MWEZI KUPUNGUZWA BEI,HII NI KIINI MACHO KUTUDHULUMU,NA HAKUNA WA KUTUTETEA

    ReplyDelete
  2. Hakika Ewura wamesalimu amri kwa vigogo wa mafuta,maana hata huko mwanzo bei ya dola ilikuwa inapanda na kushuka lakini mafuta hayajafikia bei hii,maana hapo awali bei ya petrol vituoni ilikuwa 2,060 mpk 2,080 ila Bp pekee ndio alikuwa anuza 2,215 au 2,210.Sasa hapa ni kuonyesha wazi wamwasaliti wananchi lakini bora ya haya mradi mafuta yapatikane kuliko waliporuhusu kwa maksudi kabisa ulanguzi urudi rasmi,Huu ni mtihani kwani mafuta yaliyopo yanatosha Petrol siku 48,diesel siku 32 mafuta ya taa siku 60 sasa iweje bei hii mpya imehusisha na hayo yaliyopo?
    Aah yetu macho,mla mlaleo mla jana kala nini?

    ReplyDelete
  3. Nakumbuka siku moja Bungeni Spika Makinda aliwahi kunukuliwa akisema " Ili swali sijui analijibu nani maana hii wizara ni JACK OF ALL TRADE, ina majukumu mengi sana"
    Mimi kwanza nin mashaka na uwezo na uelewa wa spika wetu mtukufu,kwa waliobaatika kusoma hiyo lugha JACK OF ALL TRADE ni JACK OF ALL TRADE BUT MASTER OF NONE,ni msemo au nahau ikimaanisha kuwa anataka kufanya mengi kwa pamoja matokeo yake yote yanamshinda.Hiyo ndiyo nahau sahii kwa wizara ya Nishati kwa msemo wa Makinda,IT IS JACK OF ALL TRADE BUT MASTER OF NONE, wizara imewsahinda,madini wao,nishati wao,labda watenganishe izo wizara.

    ReplyDelete
  4. haya ndio maisha bora kwa kila fisadi.

    ReplyDelete