Na Zahoro Mlanzi
WAKATI mabingwa wapya wa mashindano ya Kombe la Kagame, timu ya Yanga ikitarajiwa kuondoka leo kwenda Dodoma kwa ajili ya kuwaonesha wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kombe hilo, wachezaji Hamis Kiiza 'Diego' na Haruna Niyonzima 'Fabregas' hawatakwenda.
Mbali na wachezaji hao, Davies Mwape naye huenda akaikosa safari hiyo endapo atashindwa kutua Dar es Salaam leo akitokea kwao Zambia.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema baada ya safari hiyo kuahirishwa wiki iliyopita kutokana na wachezaji wao kwenda mapumziko mafupi, sasa safari hiyo imekamilika na wanaondoka leo muda wowote.
"Kama unavyojua waheshimiwa wabunge ambao ni wanachama na wakereketwa wetu wametuomba tukawaoneshe kombe letu la Kagame, tulililitwaa hivi karibuni pamoja na kubadilishana mawazo na wachezaji.
"Tutaondoka na kikosi chetu kilichotwaa ubingwa huo ambacho kina wachezaji 20, pamoja na viongozi wanne kwa jumla tunakwenda na timu yetu tulioisajili kwa ajili ya msimu ujao," alisema.
Alisema lakini katika safari hiyo wachezaji Kiiza, hatokwenda kutokana na kutua nchini leo au kesho, Niyonzima pia hatokuwepo kutokana na kuwa mgonjwa lakini hali yake inaendelea vizuri huko kwao Uganda.
ASendeu alisema Mwape naye anaweza kuikosa safari hiyo kwani aliahidi kurudi jana au leo na kwamba akichelewa itabidi abaki Dar es Salaam na atajiunga na wenzake pindi timu itakaporejea kutoka bungeni.
Akizungumzia suala la usajili hususani kwa wachezaji waliowatoa kwa mkopo kwenda African Lyon, kama wameshawasilisha barua rasmi za makubaliano ya pande tatu, alisema tayari wameshafanya hivyo na hawawezi kuwatoa wachezaji bila kuwepo kwa makubaliano.
Kabla ya Sendeu kuzungumza, Mratibu wa ziara hiyo maalumu, Cellina Agustino alisema kesho wachezaji wa hao wakiwa na kombe hilo wataingia bungeni.
Alisema mara baada ya tafrija fupi itayakayofanywa na wabunge hao, wachezaji wa Yanga jioni watafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Jamhuri na Jumamosi watakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma.
Mratibu huyo alisema kupelekwa kwa kombe hilo bungeni ni ombi la wabunge, baada ya Tanzania kufanya vizuri katika mashindano hayo, ikiwa ni pamoja kulibakisha kombe hilo nchini.
"Mechi hiyo ya kirafiki lengo lake ni kwa wakazi wa Dodoma kuiona timu yao, ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Kagame," alisema.
No comments:
Post a Comment