18 July 2011

Umaskini unachangiwa na viongozi wa CCM - Lema

Na Severin Blasio, Morogoro

MBUNGE wa Arusha Mjini Bw. Godbress Lema (CHADEMA), amesema baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanawadanganya Watanzania kwa kusema
uongo ambao matokeo yake ni kuongeza umaskini katika jamii.

Bw. Lema aliyasema hayo juzi wakati akihutubia mamia ya wananchi mjini hapa na kuongeza kuwa, uwongo huo umesababisha Watanzania kuishi kama wakimbizi katika nchi yao.

“Viongozi waongo ndani ya CCM ni pamoja na Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda alisema uwongo katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo Bungeni mjini Dodoma, alipotakiwa kutoa msimamo wa Serikali juu ya sakata la mauaji ya raia mjini Arusha,

“Nilisimama bungeni na kusema Waziri Mkuu Bw. Pinda muongo wenyewe mnajua na wameshindwa kunichukulia hatua, hivi sasa Watanzania tunaishi kama wakimbizi katika nchi yetu, ufisadi, dhuruma, wizi, upindishaji wa sheria ni jambo la kawaida huku tukujigamba tuna utawala wa sheria,” alisema Bw. Lema

Aliongeza kuwa, kama kuna watu wanadhani wapinzani wameingia katika siasa kwa lengo la kuuza sura wabadili fikra zao kwani CHADEMA itahakikisha haki za Watanzania hazipotei.

Akizungumzia kujiuzuru kwa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, Bw. Rostam Azizi (CCM), Bw. Lema alisema kujiuzuru kwake kumetokana na shinikizo la CHADEMA.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa na Mbunge Viti Maalumu Bi. Suzani Kiwanga, alisema Mkoa huo wenye neema rasirimali nyingi wananchi wake wameendelea kuwa maskini kutokana na uongozi mbovu usiojali maslahi ya walalahoi.

“Mkoa wetu umezungukwa na mabonde yenye mito ya maji yanayotosha kufanya kilimo chenye tija, madini, mbunga za wanyama, milima, wadudu, ndege na wanyama mbalimbali lakini rasirimali zote zinawanufaisha watu wachache.

“baada ya kumalizika kwa kikao cha bajeti, tumeazimia kufanya maandamano katika mikoa yote nchini ili Watanzania wajue nini tumekiona na tunataka kifanyike kwa maslahi ya nani,” alisema.

1 comment:

  1. Ni kweli kabisa umasikini wa watanzania unatokana na uongozi mbovu uliopo sasa.

    ReplyDelete