Na Gladness Mboma, Dodoma
SERIKALI imemsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. David Jairo anayedaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa, ili Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) aweze kulifanyia uchunguzi suala hilo.
Uamuzi huo wa serikali, ulitangazwa jana mjini hapa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phillemon Luhanjo alipozungumza na waandishi wa habari, huku akiweka bayana kuwa uchunguzi huo wa awali unaanza leo na utakamilika baada ya siku 10.
“Nimeona niwaambie hili ili tusiendelee kuwaambia wananchi tunamsubiri Rais, wakati mimi mwenyewe mwenye kusimamia nidhamu nipo hapa, nimeshachukua hatua.
“Kutokana na uzito wa jambo hili, nimelazimika kumwamuru CAG, Bw. Ludovick Utoah kufanya uchunguzi ndani ya siku kumi na iwapo itabainika kuwa ana makosa, hatua nyingine za kisheria zitafuata. Kwa sasa anaenda likizo ya malipo kupisha
uchunguzi,” alisema.
Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kusisitiza kuwa Rais Jakaya Kikwete anasubiriwa kutoka safarini Afrika Kusini, ili kutoa maamuzi juu ya Bw. Jairo.
Kauli hiyo ni ya pili kwa Bw. Pinda kuhusu suala hilo, baada ya kulieleza bunge kuwa lingekuwa ndani ya mamlaka yake angelimaliza siku hiyo hiyo kwa kumtimua.
Lakini jana, Bw. Luhanjo alisema akiwa Mamlaka ya Nidhamu, ameanzisha uchunguzi huo wa awali kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo.
“Kama mnavyofahamu, Julai 18 Julai mwaka huu wakati wa majadiliano ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya waheshimiwa wabunge wakati wakichangia hotuba hiyo walimtuhumu Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuhusika na tuhuma
mbalimbali.
“Baadhi ya tuhuma hizo ni kuzitaka taasisi, vitengo na idara zilizo chini ya wizara hiyo zichangie sh. milioni 50 kila moja, ili fedha hizo zitumike kuwalipa wabunge ili kufanikisha mawasilisho ya bajeti ya wizara, na kuwalipa masurufu ya
safari watumishi walio chini ya wizara na taasisi zake ambao tayari walishalipwa na wizara na taasisi zao,” alisema.
Alisema baada ya uchunguzi wa awali zipo hatua ambazo zitafuata ambapo alisema kuwa hatua hizo zitategemea matokeo ya uchunguzi huo wa awali ambapo kama atakutwa na hatia atapewa hati ya mashtaka.
Alisema lengo la kufanya uchunguzi huo ni kutaka kumpa fursa ya kujitetea kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma.
“Katibu Mkuu alituhumiwa na wabunge, na yeye hana nafasi ya kujitetea ndani ya ukumbi wa bunge, na ni lazima tuhuma zipate maelezo ya upande wa pili na hapa ndipo sheria hii ya Utumishi wa Umma inachukua nafasi yake,” alisema.
Akielezea sheria za utumishi wa umma, Bw. Luhango alisema wakati wa kipindi cha uchuguzi, mtumishi wa umma anayetuhumiwa anaweza kupewa likizo ya malipo, ili kupisha uchunguzi au akaruhusiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa.
Alisema baada ya uchunguzi huo kukamilika na kama utabaini makosa ya kinidhamu, mamlaka ya nidhamu itampa mtumishi taarifa za tuhuma ambayo itaambatana na hati ya mashtaka na kwamba wakati huo mtumishi atasimamishwa kazi na kulipwa nusu mshahara.
Tuhuma za Bw. Jairo huyo kuhusishwa na vitendo vya rushwa, ziliibuliwa bungeni na mbunge wa Kilindi (CCM), Bi. Beatrice Shellukindo baada ya kuwasilisha barua iliyoonesha mpango wa kukusanya sh. bilioni moja kwa ajili ya kuwalainisha wabunge na watu mbalimbali ili bajeti ya wizara hiyo iweze kupitishwa na bungeni.
Pinda abanwa bungeni
Waziri Mkuu Pinda jana alibanwa bungeni kutokana na kushindwa
kumwajibisha Bw. Jairo anayehusishwa na vitendo vya rushwa katika upitishwaji wa bajeti ya wizara hiyo.
Mbunge wa Tumbe (CUF), Bw. Rashid Ally Abdallah alisema
kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais ana mamlaka ya kufanya kazi za rais endapo rais hayupo, na kuhoji,pale Waziri Mkuu aliposema hana mamlaka ya kumwajibisha Bw. Jairo haoni ni kwenda kinyume na katibu hiyo?
Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alikiri mbunge huyo kumpa mtihani asioutarajia na kukiri kuwa endapo hata Makamu wa Rais asingekuwapo yeye angeweza kuchukua mamlaka ya kufanya kazi za rais.
“Mheshimiwa Abdallah umenipa mtihani wala sikutegemea. Ni kweli rais asipokuwapo na hata Makamu wa Rais, mimi naweza kukwaa mamlaka hayo, lakini kwa mujibu wa katiba hiyo hiyo si kila jambo tuna mamlaka ya kuchukua hatua. Hatuwezi kutoa msamaha wa
wafungwa. Tuna kikomo cha mamlaka,” alisema.
Alisema kuwa hata Makamu wa Rais anaweza kuchukua majukumu mengine ya rais, endapo atapata ushauri wake wakati rais hayupo.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alisema kwa mtazamo wake suala la Bw. Jairo si zito, hivyo kushauri kufanyika marekebisho ya katiba ili viongozi hao wawe na mamlaka hiyo.
Waziri Mkuu alijibu kwa kifupi, “Naheshimu mawazo yako, naomba majibu yake yabaki yale yale”.
Huyu Waziri Mkuu anaelewa anachokifanya au anabangaiza tu. Kama anaelewa Serikali inavyofanya kazi kwanini ilimbidi amwendee rais kupata mwongozo wakati mkuu wa makatibu wakuuu yupo na anao uwezo huo. Wakati mwingine huyu mtoto wa mkulima ananishangaza.
ReplyDeleteKwani hizo si show tu, kuna mchezo kamili umejificha! Luhanjo kaonyesha ubavu, lakini tutaona mwisho wake!
ReplyDeleteHatua aliyochukua Luhanjo ni sawa, pamoja na kwamba imechukua muda kufanya uamuzi na kuutoa hadharani. Ni sawa akae kando wakati uchunguzi unafanywa. Iwapo ana hatia hatua zichukuliwe; kama hana basi. Lakini tusimhukumu hadi ukweli utakapojulikana, ingawa huo mtindo wa kukusanya pesa kutoka idara na taasisi za wizara kwa ajili ya kupitisha bajeti unatia shaka na unaleta wasiwasi wa jinsi nchi yetu inavyoendeshwa.
ReplyDeleteHata huyo CAG anaweza amriwa atengeneze repoti safi ya kumsafisha fisadi. Kwani hata yeye si mtumishi tu ambaye anaweza kupokea maagizo kutoka kwa wakubwa na akafunika mambo. Tungojee tuone.
ReplyDelete..Nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.Kuna haki nyingi kama utaratibu hautafuatwa serikali itashitakiwa na kulipa.Huwezi kumfukuza tu jairo kwa maneno ya mtu lazima uchunguzi wa kina ufanyike.Hata Mungu alipompa Adama na Hawa adhabu aliwapa nafasi ya kujitetea kwanza.
ReplyDeleteHaya nimabo ya sheria sio ya nyumbani kwa pinda au waandishi wa habari.
KIKWETE NA SERIKALI YAKE NI WALA RUSHWA TU. JAIRO AFUKUZWE NI HAKI YAKE. LAKINI NGELEJA NA MALIMA HASWA NDIO WANGETAKIWA KUFUKUZWA ON THE SPOT KWANI BUDGET INGEPITA INGEWAFAIDISHA WAO (MAWAZIRI) ZAIDI. UKWELI WA MUNGU NI KWAMBA MAWAZIRI NDIO WENYE DILI. JAIRO KWA KUJIAMINI KWAKE KWAMBA ANATOKA IKULU, NDIO KAJIANDIKIA TU. NA TUJUE MPAKA KIKWETE KAMWEKA HAPO NI KWA MASLAHI BINAFSI WALA HAKUNA JINGINE. NA WALA SITASHANGAA UTOUH NA LUHANJO KUMSAFISHA JAIRO. NA SITASHANGAA BEATRICE SHELUKINDO AKIITWA MZUSHAI NA HATA KUPEWA ONYO NA SPIKA. NGOJA TUONE. KIKWETE SI RAIS NI MCHUMIA TUMBO TU!!MASIKINI PINDA UNABEBA ZIGOOOO HALIBEBEKI. SITASGANGAA HATA SIKU MOJA NGELEJA AKIWA WAZIRI MKUU. SO SAD TANZANIA.
ReplyDeleteJamani someni barua inayodaiwa ina rushwa ndani yake muelewe. Hata mtoto wa chekechea akisoma atakwambia hajaona hata rangi wala harufu ya rushwa. Nchi hii inaongozwa kwa sheria tusimhukumu huyu mtu bila kumsikiliza, uchunguzi ufanyike hata kama utafanyika jibu sahihi ni kwamba HAKUNA MTOTO WA RUSHWA WALA BABA AU BABU YAKE NA RUSHWA ATAKAYE PATIKANA. Tutumie ubongo ktk kujadili suala hili tusitumie MAKAMASI.
ReplyDelete