17 June 2011

TBS yazuia dizeli hatari bandarini

Na Rachel Balama

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limezuia shehena ya mafuta ya dizeli yenye ujazo wa tani 5,000 kuingia nchini kutokana na kutokidhi viwango vya ubora unaotakiwa
kwa kuwa yakitikisika yanaweza kulipuka.

Akizungunza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TBS Bw. Charles Ekelege, alisema shehena hiyo iliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam Juni 13, mwaka huu kwa meli ya MT. Gulf Jumeirah kutoka Falme za Kiarabu bado ipo bandarini Dar es Salaam.

Bw. Ekelege alisema wameitaka kampuni iliyoagiza mafuta hayo  kuyarudisha yalikotoka kwa kuwa yakitikisika kidogo yanaweza kulipuka.

Alisema TBS ilipima sampuli ya mafuta hayo kutoka kwenye shehena hiyo na kubaini kuwa halijoto ya mwako (flash point temperature) ya mafuta hayo haikidhi matakwa ya kiwango cha Tanzania.

Bw. Ekelege, alisema matokeo ya vipimo hivyo vilionyesha kuwa halijoto hiyo ya mwako ni nyuzi joto 56C wakati kiwango kinachotakiwa kwa Tanzania ni nyuzi joto 66C.

Alisema halijoto inahusiana na uwezo wa mafuta kulipuka au kutolipuka endapo utatokea mtikisiko wowote hususan wakati wa usafirishaji.

Halijoto ya mwako ni kigezo muhimu katika kutathmini ubora wa mafuta kwani kutokidhi kigezo hicho kunaweza kusababisha maafa wakati wa usafirishaji wa mafuta.

Alisema waigizaji wote wa mafuta wanapaswa kuhakikisha mafuta yote yanayoingizwa katika soko la Tanzania yanakidhi matakwa ya viwango vya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Shirika hilo linamtafuta mwagizaji wa pombe kali aina ya GORDON'S ambayo imezagaa mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro ili kuelimishwa matakwa ya kiwango cha bidhaa hiyo.

Bw. Ekelege, alisema pombe hiyo imepimwa ubora na kuonekana kukosa maelezo muhimu kwenye vifungashio.

Alisema maelezo hayo muhimu ambayo hayakuainishwa kwenye vifungashio vya pombe hiyo ni pamoja na tarehe ya kutengenezwa, namba ya kiwandani na usajili na kwamba wanahisi kinywaji hicho kuingizwa nchini kwa njia za panya.

1 comment:

  1. jamani tbs kulikoni mafuta yasafirishwe mwendo mrefu toka falme za kiarabu hadi hapa Tz bila kulipuka? Au meli iliyoleta shehena hiyo ilitulia na hivyo mafuta hayo hayakutikisika?Jamani tuache visingizio visivyoingia akilini

    ReplyDelete