17 June 2011

Mzimu wa Balali waibuka bungeni

Tumaini Makene na Pendo Mtibuche

ZAIDI ya miaka mitatu tangu kufariki kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Daud Balali katika wakati ambao alikuwa akiaminika
kuwa 'shahidi muhimu' juu ya wizi wa fedha za EPA, utata juu ya kifo chake umeibuka tena bungeni, mara hii mbunge akitaka serikali ioneshe mkanda wa video kuthibitisha kuwa kweli alikufa.

Mbunge huyo alitaka ushahidi wa namna hiyo ili kuzuia kile alichodai kuwa ni vitendo vya watu kudaiwa kufa baada ya upotevu wa fedha za umma na ushahidi kuishia hewani.

Kifo cha Dkt. Balali, aliyefariki huko Washngton, Marekani Mei 16, 2008, kwa mujibu wa taarifa ya serikali, kilitokea wakati sekeseke la kashfa ya EPA likiwa limepamba moto, ambapo yeye alidaiwa kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakijua njama na taarifa muhimu za namna upotevu wa fedha hizo ulivyofanyika na nani walikuwa wahusika wakuu.

Tangu kutokea kwa kifo hicho, serikali imekuwa katika wakati mgumu wa kuaminika mbele ya jamii, juu ya utata huo, baada ya kuwa imekiri mapema kuwa ilikuwa haijui hospitali aliyolazwa, wala eneo hasa alilokuwa akiishi aliyekuwa Gavana wa BoT, ambaye alikuwa amefukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete.

Serikali awali ilikuwa imekiri kuwa Dkt. Balali alikuwa ni mgonjwa na yuko kwenye matibabu nchini Marekani, lakini ilikataa kueleza yuko katika jimbo gani, wala haikutoa taarifa juu ya maendeleo ya hali yake hadi ilipodaiwa kuwa amefikwa na mauti.

Pamoja na kudaiwa kufikwa na mauti yake Mei 16, 2008, serikali, baada ya masawali mengi na usumbufu kutoka kwa waandishi wa habari, ilitoa taarifa juu ya Dkt. Balali siku tano baada ya kifo chake, hali iliyoibua maswali mengi, kwa nini serikali haikuwa ikijua mahali alipokuwa mtu muhimu kama yule.

Akiuliza swali hilo jana bungeni katika kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Mtambalile, Bw. Masoud Abdallah Salim (CUF) alidai kuwa kumekuwepo na tabia ya watu kufanya ufisadi dhidi ya mali za umma, kisha tuhuma hizo za kuiba fedha zinaishia
hewani na watuhumiwa wakidaiwa kufa.

“Tunataka serikali itoe tamko kuhusu kifo cha Balali...kama kweli alikufa basi tunaitaka serikali itoe mkanda wa video kuthibitisha hilo ili isiingie kwenye historia kama ya waliozikwa baharini," alisema Bw. Salim.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Gregory Teu alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania huko Marekani, serikali inajua Bw. Balali alikufa na kuzikwa nchini humo.

“Taarifa tulizoletewa kutoka ubalozi wetu Marekani zilisema Balali alifariki na kuzikwa huko huko, hivyo ni kweli Balali hatutamuona tena, alikufa na mambo yote amekufa nayo," alisema Bw. Teu.

Akijibu swali la msingi awali, Bw. Teu alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2009/11 matokeo ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yalionesha kuwepo kwa viashiria vya uzembe, wizi au ubadhirifu ambapo huwasilishwa kwenye taasisi husika za serikali zenye mamlaka kwa ajili ya hatua au uchunguzi zaidi wa kitaalamu na uthibitisho kwa mujibu wa taratibu wa sheria zilizopo.

Aliongeza kuwa tangu serikali ilipopokea taarifa ya CAG mwaka 2009/10 imeanza kuchukua hatua zinazostahili, ikiwemo kufikisha taarifa kwenye vyombo kama vile Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

“Katika mwaka 2008 hadi mwaka 2010 wakurugenzi wa halmashauri 73 walifukuzwa kazi, na katika mwaka 2006 hadi mwaka 2010 halmashauri 33 zilichukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kufikishwa mahakamani.

“Kuna sehemu zingine Waziri Mkuu amewahi kuingilia kati...alikwenda Bagamoyo na akachukua hatua na mwaka huu mmeona halmashauri tatu zimeadhibiwa ambazo ni Kilosa, Rombo na Kishapu," alisema Bw. Teu.

Katika swali lake la msingi, Bw. Masoud alitaka kujua kiasi cha fedha ambacho kilihusishwa na uzembe, wizi na ubadhirifu kwa mujibu wa ripoti ya CAG katika kipindi cha Januari 2009 hadi Oktoba 2010 na hatua walizochukuliwa wahusika.

4 comments:

  1. Serikali hiyo hiyo ilisema haitambui Balali yuko wapi! lakini mara ikatujuvya kuwa kafa spitalini Boston US! hivyo ni vituko vinavyohitaji maelezo ya kina!

    ReplyDelete
  2. Siamini Balali kafa. Huo ni usanii wa chama na serekali yaka ambayo imevaa ufisadi, uongo na usanii mwengi. Why shoud Bilali's death be shrouded in mystery and misinformation? Hao hao viongozi na mafisadi wao waliopanga na kutekeleza EPA, Twin Towers, Kagoda, Deep Green na uchafu mwingine mwingi ndio wajuao ukweli kuhusu Balali. Katika hii miaka mitano na nusu tumekua tunaishi katika kipindi cha giza, uchafu na mnuko ambao haujawahi kutokea tangu uhuru. Lakini kila maovu yana mwisho wake.

    ReplyDelete
  3. TUJUE KWAMBA TUNAONGOZWA NA KUNDI LA WAFALME MAANA MFALME ANALOSEMA HALIPINGWI KWA HIYO NDIO HIVYO, NI MTU KAMA HUYO BALALI AZIKWE TU KAMA KUKU ISIJULIKANE KABULI WALA PICHA ZA MSIBANI WAAAWAAA ACHENI HAYO HIYO SIO DEMOKRASI YA URAISI NI YA KIFALME NI KWELI KABISA HUKU DOG AKIFA ANAKUMBUMBU YA KABULI ITAKUWA BINAADAM, KWELI INAUMA IKIWA UNAMFANYA MWEZAKO KIPOFU?AU UMEVISHA MIWANI YA MBAO,VIONGOZI MNATAKIWA KUWAELEZA WANANCHI KIUFASAHA NINI KINAFANYIKA ILI KILA MMOJA KWA UPANDE WAKE ARIDHIKE MSIONYE UBAVU WENU WA ROYAL SIO VIZURI NA KAMWE MTAKUWA WATUMWA WA WAZUNGU MPAKA KABULINI,MUNGU IBARIKI TANZANIA.

    ReplyDelete
  4. Ni kweli kabisa hiki ni miongoni mwa viini macho vingi tufanyiwavyo na viongozi wetu, wito wangu kwa waandishi wa habari ninyi ndio tegemeo letu la kufichua habari nzito zilizojificha hivyo chapeni kazi mtupe habari kamili, pekueni sana hata kwa kuwatafuta ndugu wake wa karibu kupata ukweli- kwani hakuwa na ndugu huyo?

    ReplyDelete