16 June 2011

Dkt. Rwakatare amtaja shetani kujitetea

Na Dunstan Bahai

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi imekataa kupokea nakala ya fomu za Mchungaji Dk. Getrude Rwakatare za kujaza mali zake kwa maelezo kuwa mchungaji huyo
hakuzirejesha fomu hizo wakati muafaka na kwamba analidanganya Baraza la Maadili.

Mchungaji ambaye alifikishwa katika baraza hilo jana na kuhojiwa ni kwa nini hakujaza fomu hizo na kuzirejesha katika Tume ya Maadili, alisema labda fomu alizojaza ziliangukia mikononi mwa shetani.

Kwa mujibu wa Mchungaji huyo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Novemba 15 mwaka jana alipata fomu hizo kutoka kwa maofisa wa Tume ya Maadili akiwa bungeni na kuzijaza na kisha kuzirejesha Novemba 18 katika ofisi za Spika lakini alishangaa kupelekewa barua ya kuitwa kwenye baraza, barua aliyoipata Juni nane mwaka huu.

Alisema suala la kujaza fomu hiyo ni kitu ambacho anauzoefu nacho tangu aingie bungeni miaka minne iliyopita na kwamba suala la kujaza halichukui hata dakika 10.

Kabla ya kutoa maelezo hayo, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Bi. Getrude Cynacus alimkumbusha mbunge huyo kuwa, kwa mujibu wa sheria ya maadili, bila sababu ya msingi alishindwa kutoa tamko la rasilimali zake na watoto wake wasiozidi miaka 18 na ambao hawajaoa au kuolewa.

Mwanasheria huyo alisema pamoja na kumtumia mbunge huyo fomu hiyo, alikaidi kuijaza licha ya kumuandikia barua ya kumkumbusha.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni sababu ya kutojaza fomu hiyo ambayo haichukui hata dakika 10, iweje tuweze kufanya mitihani hata ya chuo kikuu na kufaulu leo hii nishindwe kujaza fomu hii. Huu siyo mtihani," alihoji.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, baada ya kukabidhiwa fomu hizo bungeni walitia saini kwenye daftari maalumu lakini alipomaliza na kuzirejesha kwa Spika, hakuna mahali waliposaini.

Hata hivyo mwanasheria huyo wa sekretarieti ya maadili alionekana kumshambulia mbunge huyo kwa maswali mazito hadi Jaji Mstaafu Damian Lubuva ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo kuingilia kati.

Mahojiano kati ya mwanasheria huyo na mbunge huyo yalikuwa hivi:

Mwanasheria: Mheshimiwa Mchungaji, umesema unafahamu matakwa ya kiongozi kutoa tamko.

Mchungaji: Ndiyo, na nilikuwa nikitoa mwaka hadi mwaka.

Mwanasheri: Unasema ulipozirejesha fomu zako hukusaini popote, kwa nini.

Mchungaji: Kwa sababu kulikuwa na foleni ya wabunge na kila mtu alikuwa anarejesha na mimi nilikuwa na haraka.

Mwanasheria: Mchungaji unasema uongo, kwa nini hukusaini, sekretarieti itakuamini vipi, kwani hata hiyo nakala ni ile fomu ambayo uliichukua halafu hukuirudisha au katika ofisi za bunge ulikorejesha kuna mtu anakuchukia ndiyo maana hakuirejesha sehemu inakohusika.

Mchungaji: Hapana, lakini inawezekana ilifika mikononi mwa shetani. Nilikuwa sina wasiwasi nilijua zimefika na niko salama kwani suala hili ni sawa na mtu anajiona yuko ndani ya nyumba lakini kumbe yuko nje na simba anakuja kumkamata.

Mwanasheria: Unasema ofisi ya Spika ndiko ulikokabidhi, mbona ndiyo waliotuletea majina yenu au unataka kutuambia ofisi hiyo hawako makini na kutunza kumbukumbu.

Mchungaji: Mimi sisemi kama kuna hujuma, ila ni shetani tu.

Mwanasheria: Unazungumzia shetani kila mara, huyu shetani ni nani.

Mchungaji: Ni roho chafu.

Mwanasheria: Ndani ya dunia hii ya sayansi unaweza kuamini hayo.

Mchungaji; Ndiyo, yupo huyu shetani na kama Mungu angeshuka leo hii angesema ukweli kuwa nimerudisha fomu hizo.

Wakati mwanasheria huyo akiendelea kulishawishi baraza lisiamini utetezi wa Mchungaji huyo kwa kusisitiza kuwa nakala hiyo fomu yake iko nyumbani kwa Mchungaji ambayo hakuirejesha kwenye tume.

Kauli hiyo ilimlazimu Jaji Lubuva kuingilia kati kuwa anachozungumza mwanasheria huyo ni tuhuma na hana ushahidi wowote, hivyo aendelee kuuliza maswali ya msingi ingawa mwanasheria huyo alisisitiza kuwa ni ukweli kwani hakuna nakala halisi, aliendelea na maswali.

Mwanasheria: Unasema ulikwenda kwenye ofisi ndogo za Tume ya Maadili pale Dodoma, je, ulijitambulisha kwa maofisa wa Tume?

Mchungaji: Ah! sikujitambulisha, wananijua si unajua mimi ninafahamika sana, nilipofika tu pale walianza kuniita, 'mchungaji,  mchungaji, bwana asifiwe!

Mwanasheria; Lakini Mchungaji mimi sikufahamu!

Mchungaji: Ah! leo si ndiyo wajina umenifahamu? (Mwanasheria huyo anaitwa Getrude).

Hata hivyo, mwanasheria huyo aliliomba baraza kutupilia mbali utetezi wa mbunge huyo na kumchukulia hatua kali.

Hata hivyo, Mchungaji Rwakatare aliendelea kujitetea, "Mimi nimerudisha fomu hizo Mungu ni Shahidi".

Baada ya kumalizika kwa utetezi huo, Jaji Lubuva alisema baraza litatoa mapendekezo kwa upande mwingine unao husika kwa hatua zaidi.

Baada ya hatua hiyo Mchungaji Rwakatare aliwainamia wanasheria na kisha meza ya majaji na kutamka "Mungu awabariki sana" kisha kutoka nje.

Mbunge mwingine aliyefikishwa jana katika baraza hilo ni Bw. Moshi Kakoso wa Mpanda Vijijini (CCM) ambaye naye anasubiri uamuzi wa baraza.

Pindi wabunge hao watakapopatikana na hatia, adhabu wanazostahili kuzitumikia ni kufukuzwa kazi (Ubunge), kushushwa cheo, kujiuzulu au kuonywa.

Kwa mujibu wa orodha ya viongozi wa umma watakaofikishwa kwenye baraza la madili, hadi Juni 24, mwaka huu ni 23 wakiwemo wabunge tisa, sita kati yao tayari wamekwishahojiwa. Watatu waliobaki na Mbinga Magharibi (CCM), Bw. John Komba na wa Hai (Chadema), Bw. Freeman Mbowe.

Wengine ni madiwani, wakurugenzi, mahakimu, majaji na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Bw. Abdul Cisco Mtiro.

Baraza hilo linaongozwa na Jaji Mstaafu Lubuva akisaidiwa na Jaji Mstaafu Khamis Msumi na Katibu Mkuu Mstaafu Bw. Gaudios Tibakwatila.

7 comments:

  1. Yawezekana Mchungaji alirudisha ila tu ni kutokusaini kumeleta tatizo. Ila kwa ushauri mangu siku nyingine asikubali kufanya jambo ambalo linahitajika kusaini akaacha akiamini kufahamika kwa kuwa ni mchungaji itamsaidia. Sheria haichagui. Wenye nia mbaya hutumia mwanya huo kumdhalilisha/kumuaibisha mtu.

    Mungu atakushindia Mchungaji kama kweli ulirudisha. Shetani ni mjanja sana ila ukishamjua ujanja wake hafurukuti atashindwa na atakukimbia tu. Bwana akubariki

    ReplyDelete
  2. Rwakatare mjanja na ni tapeli wa kutupwa; asidanganye watu kuwa alirudisha fomu. Anaogopa kutaja mali alizonazo maana ni za kitapeli tu. Alianza madini, Madawa ya kulevya, kuwatapeli akina mama vyerehani 170, shule za kitapeli kwa kuwalipa wakenya isivyo halali, kuanzisha kanisa na kununua mali za serikali kwa bei ya bwerere. Mfano. Mashine/ kiwanda cha Mlimba. Aidha, ni mhuni wa kukwepa kodi kwa kuhonga sana tu. Vibali vya wafanyakazi wageni kwake ni ndoto; pesa tu ndo siri ya mambo yote. Huyo ndiye Getrude Pangalile Rwakatare - Mpogoro tapeli na kawashika wanaume pabaya. Mchungaji feki!! Hatumuwezi. Ukiingiza dini ndiyo kabisaaaa, hashikiki. Mashavu tu kukuwa kama hana akili nzuri vile!!!! Asiwadanganye chochote huyoooo, Mwizi tuuuuu. Anaiharibia CCM tu kwa sasa, maana hata bungeni hachangii mijadala. Kama sio kuutaka ubunge ili awe na kinga ya uovu ni nini?????? Serikali KALAGABAHOOOOOO!!!!!!!!

    ReplyDelete
  3. Chris,nayasapoti uliyoyaandika hapo juu.Watu kama hawa wanaotumia vivuli vya siasa,dini na n.k kuuhadaa uma inabidi tuwachinjilie mbali. Kwa maana hiyo tusikubali wezi,waongo na wadhulumati kama hao eti watudanganye wanatangaza neno la mungu. Kuna baadhi ya dini zimeanzishwa kimaslahi zaidi,Ushirikina mwingi.Mfano ni huyo muongo,Zachari Kakobe,Nabii Malisa{mwanza},baba Godi[mwanza] na wengine hasa hasa madhehebu ya kikristo.

    ReplyDelete
  4. Please Chris; nakushangaa na nakukusikitikia sana juu ya kauli zako!Angalia mdomo uliponza kichwa.kwa sasa unaongeabila kujali yakutokayo kinywani, lakini utajajuta kwa kauli zako hizo,mie namfahamu sana Rwakatare kuliko wewe unavodhani unazifahamu habari zake; hallow, angalia sana mie sikufahamu lakini napenda kukutahadharisha mapema, huyo ni mtumishi wa Mungu unayonena juu yake yatakuangamiza iko siku isiyo na jina

    ReplyDelete
  5. Afahali ya lwakatare kuliko hao mafisadi wengine wasio hata na lepe la huruma . MUNGU atawachoma moto wote Hata huyu lwakatare ajeaangalie kama antumia jina la YESU vibaya an chance bado ya kutubu. Lakini Ole ni wake kama yanenwayo juu yake ni ya kewli kwani atachomwa kwenye tanuru la moto kwa kutumia jina la MUNGU vibaya

    ReplyDelete
  6. Huyo mama ana mshikaji dogodogo; aliwahi kumkomba hela kibao lakini wakayamaliza kiaina maana ilitaka kuwa ishu kwa wana usalama! Mama huyu anaongoza kwa kuwanyima watanzania ajira na kuwapa wakenya. halafu anawalalalia hao wakenya ile mbaya kwa kuwa wako nchini kufanya kazi bila kibali. Wambane aseme, na sie asipotaja mali zote na zile anazowashikia wengine tutamuumbua

    ReplyDelete
  7. ya mungu apewe mungu na ya kaisali apewe kaisali

    ReplyDelete