02 June 2011

Simba, Yanga kukumbana Agosti 13

Na Zahoro Mlanzi

WAPINZANI wa jadi nchini, timu za Yanga na Simba zitafungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara 2011/2012 Agosti 13, mwaka huu zitakapoumana
katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Wakati miamba hiyo ikifungua msimu mpya, pazia la ligi hiyo litafunguliwa rasmi Agosti 20, mwaka huu.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili mfululizo katika mchezo huo ambapo msimu uliopita Yanga, ilitwaa hiyo Ngao ya Jamii kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika zikiwa zimefungana mabao 2-2.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mechi za matayarisho ya msimu mpya zimeanza rasmi jana mpaka Agosti 13, mwaka huu.

"Pamoja na mechi hizo, mechi ya Ngao ya Jamii kwa ajili ya ufunguzi wa msimu kwa mikoa yote itachezwa Agosti 13, mwaka huu wakati mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom utaanza Agosti 20, mwaka huu," alisema Wambura.

Alisema mchezo huo huusisha bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa Kombe la FA, kwa kuwa hakuna mashindano ya Kombe la FA italazimika kucheza bingwa na wa pili.

Wambura alisema TFF imetoa kalenda yake ya matukio kwa mwaka 2011/2012, ambapo kipindi cha kwanza cha uhamisho kinaanza Juni Mosi hadi Julai 15, ambapo usajili wa kwanza utakuwa Juni Mosi hadi Julai 20.

Alisema kutangaza wachezaji wa kuachwa au kusitisha mikataba ni kuanzia Juni Mosi hadi 21, mwaka huu wakati kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Julai 21 hadi 31, mwaka huu.

"Kipindi cha pili cha uhamisho kitaanza Novemba Mosi hadi 20, mwaka huu wakati usajili utaanza Novemba Mosi hadi 30 na ratiba ya Ligi Kuu inatarajiwa kutoka Julai 20 na kwamba wadau wote wahakikishe wanapata kalenda hii, ili wapange shughuli zao," alisema Wambura.

Katika hatua nyingine, Wambura alisema Kozi ya Wakufunzi ya Waamuzi wa Mikoa, imeanza Dar es Salaam ikishirikisha wakufunzi 16 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Alisema wawezeshaji katika kozi hiyo iliyoanza jana na itakayomalizika Jumamosi ni Hafidh Ally, Leslie Liunda, Joseph Mapunda, Riziki Majala na Juma Ali David.

No comments:

Post a Comment