Na Raphael Okello,Serengeti
WATU 9 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwa tuhuma ya kufanya vurugu na kuvamia Kituo cha Polisi cha mjini Mugumu wilayani
humo kwa lengo la kulipiza kisasi kwa
watuhumiwa wawili walioshikiliwa na jeshi hilo.
Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Bw. Franco Kiswaka, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bw. Jackob Sanga aliieleza mahakama hiyo jana kuwa watuhumiwa hao walifanya tukio hilo juzi saa 7.30 mchana mjini Mugumu ambapo polisi walilazimika kutumia risasi baridi na mabomu ya machozi ili kuwatawanya.
Alisema watuhumiwa hao walilenga kulipa kisasi kwa watuhumiwa wengine wawili ambao hapo awali walishikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma ya kuua mtu na mke wake na kupora mifugo yao.
Alisema kundi la wananchi zaidi ya 300 kutoka katika Kijiji cha Itununu wakiwa na silaha za jadi walivamia kituo hicho saa 10 usiku wa kuamkia juzi.
Aliwataja waliofikishwa katika mahakama hiyo kuwa ni Bw.Sospeter Gaspar, Bw. Wambura Waingari, Bw.Mwita John wakazi wa mjini Mugumu Bw.Joseph Mwita na Bw.Joseph Matiko wakazi wa Kijiji cha Itununu wilayani Serengeti.
Bw. Sanga aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Bw. Franco Kiswaka, Bw. Mkora Maswi, Bw. Nyang’anyi Waitara na Bw. Peter Barnaba wakazi wa Kijiji cha Itununu ambao walisomewa wakiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti ambao wamelazwa baada ya kujeruhiwa.
Washtakiwa wote kwa pamoja walikana mashtaka na kesi yao imeihirishwa hadi juni 14 mwaka huu itakapotajwa tena hata hivyo washitakiwa walishindwa masharti ya dhamana kwa wakati huo baada ya kutakiwa kuwa
na wadhamini wawili kila mmoja.
Awali Kamanda wa polisi mkoani Mara Bw.Robert Boaz aliwataja watuhumiwa wanaodaiwa kuwachinja mtu na mke wake kisha kupora ng’ombe wao kuwa ni Bw.Mwita Magori(19) na Chacha Magori (19) ambao wote ni wakazi wa Kijiji cha Itununu wilayani Serengeti ambao nao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment