Na Addolph Bruno
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mechi ya kwanza ya mchujo ya michuano ya Olimpiki kati ya timu ya taifa ya vijana
'Vijana Stars' dhidi ya Nigeria ambapo cha juu kitakuwa 10,000 na cha chini ni Shilingi 1,000.
Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Boniface Wambura alisema viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 1,000 kwa viti vya kijani, bluu na rangi ya chungwa na sh. 5,000 kwa VIP C ambapo VIP A ni sh. 10,000.
Alisema tiketi zitaanza kuuzwa kesho saa 2 asubuhi kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Bigbon Msimbazi (Kariakoo), Steers (Mtaa wa Ohio na Samora), Uwanja wa Uhuru, Ubungo OilCom na vituo vya mauzo vya Premier Sports Betting.
Wambura alisema Nigeria itawasili kesho kama ilivyo kwa waamuzi wa mechi hiyo kutoka Kenya na Kamishna kutoka Ethiopia. Mwamuzi ni Sylvester Kirwa ambaye atasaidiwa na Peter Kiereini, Aden Marwa na Davies Omweno wakati Kamishna ni Sahilu
Gebremariam.
Wakati huo huo Wambura alisema mechi hiyo itachezwa saa moja jioni na TFF kupitia Kurugenzi ya Masoko, imepiga marufuku wachuuzi wa viburudisho kwenye mechi hiyo, isipokuwa kwa kampuni maalumu iliyopewa kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment