14 June 2011

Simba kuifuata Motema Pembe Alhamisi

Na Zahoro Mlanzi

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Simba, inatarajia kuondoka nchini Alhamisi kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kurudiana
na DC Motema Pembe katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe hilo.

Mchezo huo wa marudiano utapigwa Jijini Kinshasa Jumapili, ambapo Simba inahitaji sare ya aina yoyote iweze kuiinga hatua hiyo na moja kwa moja itaingia Kundi B lenye timu za Maghreb de Fes ya Tunisia, JS Kabylie ya Morocco na Sunshine Stars ya Nigeria.

Simba itasafiri kifua mbele mpaka nchini humo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya mchezo wa kwanza kuibuka na ushindi wa bao 1-0, uliopigwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema wataondoka Alhamisi wakiwa na wachezaji 17, pamoja benchi la ufundi na viongozi.

"Namshukuru Mungu kwa kuanza vizuri katika mchezo wa kwanza na tutarudiana Jumapili huko kwako, nina imani tutakwenda kupigana kufa au kupona kuhakikisha tunaingia hatua ya makundi," alisema Rage.

Alisema timu yao imebakiwa na wachezaji wachache, ambapo wengi wao ni majeruhi lakini ana uhakika benchi la ufundi litafanya kazi yake kwa kuwapa sapoti kubwa kuhakikisha wanafanikisha hilo.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mosses Basena akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa juzi kati ya Simba na Motema Pembe, alisema wapo katika kipindi kigumu cha kutengeneza timu.

Alisema wamempoteza Haruna Shamte (alitolewa nje kwa kadi nyekundu) lakini amerudi, Jerry Santo ambaye alikuwa na kadi mbili za njano, hivyo ana imani bado wana nafasi ya kusonga mbele zaidi.

Akizungumzia mchezo huo kwa ujumla, alisema Motema Pembe ni timu nzuri na ni ya ushindani, lakini ameona upungufu wao na ndani ya wiki moja atayafanyia kazi.

"Ni matokeo mazuri tumeyapata nyumbani kwani hivi sasa tuna wachezaji wachache ni 17 tu waliobaki hivyo tunahitaji kucheza kwa kushirikiana zaidi na niwashukuru Mgosi (Mussa Hassan) na Banka (Mohamed) kwa jinsi walivyocheza.

"Pamoja na hao lakini Kiemba (Amir) ni mchezaji wa kipekee kwani ana kipaji na ni kijana mdogo, leo (juzi) jinsi alivyocheza amenifurahisha sana kwani hakuwa na haraka ya kutoa pasi nina uhakika atakuwa mchezaji mzuri baadaye," alisema.

No comments:

Post a Comment