Na Addolph Bruno
CHUO Kikuu cha Memorial Newfound cha Canada kwa kushirikiana na Asasi zisizo za Kiserikali za Tanzania Students Achievement Organisation na Klabu ya
Kikapu ya Mambo wameandaa kambi ya mafunzo ya mpira wa Kikapu kuunga mkono jitihada za kuendeleza mchezo huo katika shule hapa nchini.
Akizungumza Dar es Salaam Jana, Kocha wa Mpira wa Kikapu wa klabu hiyo, Bahati Mgunda alisema mafunzo hayo yatahusisha vijana kati ya umri wa miaka 14 mpaka 18 ambapo yatafanyika katika viwanja vya Shule ya Kimataifa ya Tangantika (IST) Masaki jijini.
Alisema wachezaji watakaofanya vizuri katika mafunzo hayo watapata fursa ya kwenda kusoma katika chuo kikuu cha Memorial Newfound kwa kupewa msaada wa kulipiwa sehemu ya ada ya chuo hicho.
Alisema mchujo kwa wavulana utafanyika asubuhi ya Juni 20, mwaka huu mpaka jioni ambapo kwa wasichana itakuwa ni Juni 27 ambapo watakaochaguliwa kwa jinsia zote wataendelea na mafunzo Juni 21 na 24 kwa wavulana na kwa wasichana ni Juni 28 mpaka Julai Mosi.
"Washiriki wa mafunzo hayo watatakiwa kuchangia sh. 15,000 kwa ajili ya gharama za vinywaji chakula na fulana wakati wa mafunzo na tunawaomba wazazi na walimu kuwasaidia wachezaji kuja na nakala za vyeti vya kuzaliwa na ripoti za maendeleo ya masomo yao," alisema Mgunda.
Alisema Mkufunzi wa mafunzo hayo, Peter Benoite kutoka katika chuo hicho na anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam keshokutwa ambapo kabla ya kufanya lolote atazungumza na vyombo vya habari siku ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment