Na Peter Mwenda
SHIRIKISHO la Wasanii Tanzania (SHIWATA) limefikia makubaliano na Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na vifaa vya Ujenzi wa Gharama Nafuu (NHBRA) kujenga
nyumba za wasanii Mkuranga.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema Dar es Salaam jana kuwa NHBRA wamekubali kujenga nyumba za wasanii hao ambazo zitakuwa na vyumba vitatu na sebule kwa gharama na nafuu katika mashamba yao ya Mkuranga.
Alisema wanachama wake ambao ni waandishi wa habari, wasanii na wanamichezo waliojiunga na kijiji cha Mwanzega, Mkuranga katika kutekeleza sera ya Kilimo Kwanza, shirikisho hilo pia litagawa mashamba kwa ajili ya wanachama, ambao watakuwa tayari kulima msimu huu.
Taalib alisema wanachama wote wanatakiwa kuhudhuria mkutano Jumamosi saa 3 asubuhi katika Ukumbi wa Splendid Ilala, ili kupata taarifa za ujenzi na mgawo wa mashamba ya kilimo.
Alisema katika mkutano huo, wanachama wa SHIWATA ambao wamepewa maeneo yao ya Mkuranga watakabidhiwa hati za kijiji cha Mwanzega Kimbili, Mkuranga.
Mwenyekiti huyo alisema SHIWATA, inakusudia kufanya sherehe za uzinduzi wa miradi yao kijijini Mwanzega, Mkuranga Juni 25 mwaka huu ambapo viongozi mbalimbali wamealikwa na wamekubali kuhudhuria.
No comments:
Post a Comment