*Mwingine atekwa, akutwa amechinjwa
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi mkoani Dar es Salaam limeingia kwenye kashfa nyingine ya kujeruhi zaidi ya wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari Mbezi, Dar es Salaam.Majeruhi
sita wamejeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao huku mwanafunzi mmoja, Valerian Costantine akijeruhiwa shingoni kwa kitu ambacho polisi wamesema kina nchi kali.
Wanafunzi wengine sita walipoteza fahamu kutokana na kitendo cha askari kufyatua mabomu ya machozi huku wakirusha risasi za plasiki.
Tukio hilo lilitokea jana katika maeneo ya Mbezi baada ya wanafunzi wa Sekondari ya Mbezi kufunga barabara wakidai matuta ili kupunguza ajali zinazotokea katika maeneo yao.
Mapambano kati ya askari na wanafunzi wa shule hiyo yalianza nyakati za saba mchana, ambapo wanafunzi hao walifika katika Kituo cha Polisi cha Kimara kwa lengo la kuomba kibali cha kuweka matuta katika barabara ya Morogoro.
Walifikia hatua hiyo kutokana na kifo cha mwanafunzi mwenzao wa kidato cha tatu kilichotokea juzi kwa kugongwa na gari hivyo wakalazimika kufika kituoni hapo kwa lengo la kuomba kibali.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa baada ya wanafunzi hao kueleza ombi lao, askari hao waliwafukuza hatua iliyowafanya kuingia barabarani na kuziba barabara.
Kitendo cha kuziba barabara, kiliwafanya askari hao kuingilia kati kwa kufyatua mabomu ya machozi hali iliyoibua hasira kwa wanafunzi hao na kuanza kurusha mawe kwenye magari yaliyokuwa yakipita eneo hilo.
Shuhuda wetu walieleza kuwa, baada ya wanafunzi kuona wamezidiwa nguvu na askari walitawanyika na kuhamia eneo jingine la Mbezi Inn ambako waliziba barabara na viroba vya mchanga hatua iliyolifanya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kuomba nguvu ya ziada kutoka mikoa mingine ya kipolisi ya jijini Dar es Salaam.
Harakati hizo za wanafunzi ziliungwa mkono na wananchi wa eneo hilo hatua iliyowalazimu askari kurusha risasi na kusababisha majeruhi hao.
Akithibitisha tukio hilo, Mkuu wa shule hiyo, Bw. David Msuya alieleza kuwa kutokana na vurugu hizo wanafunzi sita ambao wana matatizo ya moyo walipoteza fahamu huku wengine sita wakijeruhiwa na mmoja akipata majeraha makubwa zaidi.
Alisema kuwa majeruhi hao wanatibiwa katika zahanati ya Ruguruni na uongozi wa shule umeshindwa kuwapeleka katika Hospitali ya Serikali kwa kuwa polisi wamegoma kutoa fomu namba ya tatu kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Charles Kenyela alisema wanafunzi hao wakiwa na mawe, nondo, vyuma chakavy na vipande vya matofari walifunga barabara kushinikiza kuwekwa matuta.
Alisema polisi walipofika kuwatuliza walishambuliwa na kurudi nyuma kituoni Kimara kujihami, ndipo waliajipanga na kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kurusha risasi hewani.
Kuhusu wanafunzi 12 waliojeruhiwa, alisema walifika shuleni kwao wakiwa katika hali mbaya baada ya vurugu hizo na kuripotiwa polisi na mwalimu Said Ambani na polisi walikwenda kuwachukua na kuwapeleka kutibiwa katika Hospitali ya Tumbi.
Alisema pamoja na hao 12, polisi inawashikilia wanafunzi 27 wanaohojiwa kuhusiana na vurugu hizo.
Wanafunzi achinjwa Njombe
Naye Mercy James anaripoti kutoka Njombe kuwa watu wasiofahamika wamemchinja Mwanafunzi wa Darasa la tano katika Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya Livingstone iliyopo Mjini Njombe Mkoa wa Iringa kwa kuutenganisha mwili wake na kichwa.
Tukio hilo lilitokea jana ambapo mtoto Doris Lutego (12) alichukuliwa na watu wasiofahamika baada ya kuvamia bweni la wasichana juni 12 mwaka huu saa sita usiku na kutokomea naye kusikojulikana na baadaye kukuta mwili wake ukiwa umetenganishwa na mwili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Evarist Mangalla alisema mwili wa mtoto huyo ulipatikana katika Kitongoji cha Kambarage nje kidogo ya mji wa Njombe ukiwa ndani ya mfuko wa Sandarusi (Sarufeti) huku kichwa chake kikiwa kando kwenye mfuko wake wa daftari ambao pia unadaiwa kuwa ulichukuliwa siku ya tukio.
Alisema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo ziliripotiwa juni 12 mwaka huu katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Njombe, na kwamba jitihada zinaendelea kusaka wahusika wa mauaji hayo ya kutisha.
Katika tukio jingine, mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Bi. Rehema Kadaga Mkazi wa Kijiji cha Kanamalenga Kata ya Ilembula jana alikutwa akiwa uchi wa mnyama baada ya kudondoka kwa imani za kishirikina.
Tukio hilo lilitokea katika mtaa wa Mjimwema B, katika Kitongoji cha Kitisi Mjini Makambako ambapo ilidaiwa kuwa Bi. Kadaga alikutwa katika mtaa huo saa 12 asubuhi akiwa hana nguo ambapo alipotakiwa kujieleza sababu za kuwa pale alisema, alikuwa akienda Kibena Njombe.
Akizungumza na Majira eneo la tukio jana asubuhi Bi. Kadaga alisema, alikuwa akifanya biashara ya mayai kijiji kwao ambapo alichuliwa na wenzake watatu akiwemo baba yake wakati wanasafiri yeye alidondoka na kwamba hajui amefikaje hapo alipo.
Alisema kuwa licha ya kufanya biashara hiyo pia alikuwa akilinda benki kwa miaka mingi bila kufafanua ni benki ipi na kwa ajira ya kampuni gani hata hivyo wananchi waliendelea kumzonga huku wakishangaa,na kumtembeza huku akiwa uchi hadi kituo cha polisi.
Mwenyekiti wa Kijiji, Bw. Laiza Gadau na barozi wa mtaa ambapo tukio hilo lilitokea walisema, mama huyo alikutwa mtaani hapo akiwa kama alivyozaliwa na kwamba wanachofahamu matukio kama hayo mara nyingi huhusishwa na imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi Bw. Mangalla alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi wa kina unaendelea katika matukio yote mawili.
Police violence and brutality against citizens of this country is reminiscent of apartheid South Africa of a dark era gone by.
ReplyDeleteOur police force is not only brutal, it consists of trigger-happy murderers, protectors of criminals and big-time gangsters,thieves, bribe takers, framers,and very fat-assed good for nothing types that know nothing but to mete out terror to innocent people. Phew!