02 June 2011

Nyumba za NHC Upanga hazitauzwa-Lembeli

Na Tumaini Makene

SIKU moja baada ya kuibuka kwa taarifa za baadhi ya wapangaji wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) kutaka kuuziwa nyumba katika eneo nyeti la
Upanga, jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bw. James Lembeli kung'aka, akisema msimamo juu ya suala hilo uko wazi tangu bunge lililopita kuwa hazitauzwa.

Msimamo huo umekuja kutokana na harakati za wapangaji hao kuandaa mkakati wa kuuziwa nyumba hizo, kwa kisingizio kuwa wamekaa kwenye nyumba hizo muda mrefu, huku wakiwa wamefanikiwa kuvuka 'kizingiti' cha uongozi wa NHC na kupata miadi ya kuonana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, wakati wowote kuanzia sasa.

Kwa muda mrefu sasa wapangaji wa NHC katika eneo hilo wamekuwa wakijenga hoja za kutafuta uhalali wa serikali kuwauzia nyumba zilizoko katika eneo hilo, wakitaka wafanyiwe hivyo kwa bei poa kama ilivyokuwa kwa nyumba za serikali zilizouzwa wakati wa Serikali ya Rais Benjamin Mkapa.

Hatua hiyo imekuja wakati kitendo cha kuuzwa kwa nyumba za serikali kwa serikali ya awamu ya tatu kikiwa bado kinafukuta katika mijadala ya ufisadi mkubwa nchini.

Hoja ambayo imekuwa ikitumiwa na wapangaji hao ambayo, Bw. Lembeli ameonekana kuishangaa ni kukaa kwa muda mrefu katika nyumba hizo, akisema 'hivi uliona wapi mpangaji akipanga katika nyumba yako muda mrefu tu kinakuwa ni sababu ya wewe kumuuzia nyumba yako.'

Akizungumza na Majira jana, Bw. Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama alisema kuwa suala hilo liliwahi kufikishwa katika kamati yake na hatimaye kutinga bungeni katika bunge la tisa na likawekewa msimamo kuwa nyumba hizo hazitauzwa.

"Suala hili lilishakuja katika kamati yangu...lilishajadiliwa katika bunge la tisa, msimamo wa wa bunge katika hili unafahamika. Hata juzi tulipokutana na Bodi ya NHC tuliwaambia msimamo ni ule ule."

Akitoa maoni yake binafsi alisema "kwa nini mtu anataka kung'ang'ania kununua nyumba katika eneo kama hilo...kwanza hizo nyumba za Upanga si nyumba tena. Zimechoka. Thamani ya pale ni kiwanja, ambapo kiwanja kimoja kinaweza kuwa thamani ya bilioni moja. Zile nyumba ni za Watanzania wote.

"Kukaa katika nyumba zile hakuwapatii wapangaji haki ya kutaka kuzichukua...hivi wewe uliona wapi mpangaji anapanga kwenye nyumba yako kwa muda mrefu halafu anasema kuwa amekaa sana, hivyo anastahili umuuzie."

Alipoulizwa na Majira juu ya kuwepo kwa njama zinazosukumwa na baadhi ya wafanyabiashara matajiri wanaotaka kumiliki eneo hilo, Bw. Lembeli alisema 'watajijua huko huko...itakula kwao.'

Katika kufuatilia undani wa suala hilo, Majira lilipata nakala ya taarifa ya muhtasari ya wapangaji hao kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya NHC, baada ya kuwa wamekutana na waziri, kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Oktoba, 2009.

Wapangaji hao wanadaiwa kutumia vibaya kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya Agosti 07, 2008 aliyoitoa Iringa wakati akifungua majengo ya NHC kuwa 'mtu hawezi kuishi ndani ya nyumba za NHC kwa miaka 30 bila kufaidika, huku shirika hilo likijenga nyumba zaidi kutokana na kodi za wapangaji hao' wakisema aliruhusu uuzwaji wa nyumba hiyo.

Katika mapendekezo yao yaliyosainiwa na watu wawili, mwenyekiti wa kamati Bw. Mujengi Gwao na katibu wake, Bw. Marco Rweyemamu, wapangaji hao wa Ilala wanasisitiza haki na usawa katika uuzwaji wa nyumba za NHC, wanasema wapangaji washirikishwe kikamilifu, pia ihakikishwe watu wasio raia hawapati nyumba hizo.

Pia wanataka viwango vya kodi walizokwishalipa katika nyumba hizo vihesabiwe na kupunguzwa katika bei za kuuziwa, wapangaji hao wanasema.

Wanasema "Kuna baadhi ya nyumba za NHC ambazo tayari kuna wapangaji wanaomiliki sehemu zao wenyewe (tenants purchaser) kati yao wapangaji wa NHC ni 4 hadi 5, nyumba za namna hii tunapendekeza wapangaji wote wauziwe au wamilikishwe jengo hilo na NHC iachane na mambo ya kupangisha.

"Kwamba kwa kuwa wapangaji wengine ni wajane, yatima na wastaafu hawategemei kabisa kwamba watauziwa/kumilikishwa sehemu za nyumba kwa bei au thamani ya nguvu za soko ambayo kwa masuala ya nyumba za NHC kwa kweli halipo kabisa kwa kuwa nyumba za serikali Ostabay na mikoani hazikuuzwa kwa bei ya soko wakati huo.

"Kutokana na hali/uwezo mdogo kihistoria wa wapangaji wengi wa shirika, hasa nyumba za malazi na kwa mujibu wa sheria mpya ya mikopo ya nyumba Na 17/2008 wapangaji wanaomba na watashukuru sana kuwezeshwa kwa mikopo ya fedha ili waweze kununua sehemu zao za nyumba ambazo wameishi kwa miaka mingi, ili wasiwe na shida na matatizo ya fedha.

Juhudi za kumpata Prof. Anne Tibaijuka ambaye atakutana na wapangaji hao hivi karibuni ziligonga mwamba baada ya simu zake za mkononi kuita muda bila kujibiwa.

Kwa upande wa Bw. Gwao, ambaye mbali ya kukanusha vikali madai ya kuwepo msukumo wa watu wengine katika suala hilo, alisema kuwa wana haki ya kuomba kuuziwa.

"Huo ni uongo mkubwa, that is completely nonsense, it is typical nonsense, hakuna kitu kama hicho hiyo ni nia ya kutaka kutu-undermine sisi Watanzania wazawa. Tuna haki kama Watanzania wengine kuomba kuuziwa nyumba hizo za NHC ambazo sisi tumekaa muda mrefu. Tunachotaka ni nyumba, ziko mahali gani it is non of our business,"

"Tena nia ya kuziuza nyumba hizo ilianzia kwa Rais Kikwete mwenyewe, tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya bunge...hilo ni ombi tu...hata mikataba ya kimataifa...unajua ile mikutano ya UNHABITAT inafanyika kila baada ya miaka mitatu, inasema ni haki kwa mpangaji kuuziwa nyumba kama tunavyoomba sisi," alisema Bw. Gwao.

Maombi hayo yanakwenda kinyume na mpango wa menejimenti ya NHC ambayo inasisitiza kuwa haitauza nyumba katika maeneo hayo nyeti, bali kujenga maghorofa yatakayowezesha kuishi familia 200,000 badala ya 4,000 za sasa.

Mkuu wa Kitengo cha mahusiano wa NHC, Susan Omari alisema jana kuwa shirika halina mpango wa kuuza nyumba hizo bali kujenga nyingine ambayo michoro yake iko tayari na kunzia Juni mwaka huu zabuni zitaanza kutangazwa.

Alisema mpango wa baadaye ni kuuza nyumba hizo kwa asilimia 70 na kuwawezesha watakaokuwa wanunuzi kupata hati ya kumiliki makazi ndani ya ghorofa husika huku ardhi husika ikibaki mali ya NHC.

"Baada ya ujenzi wale waliokuwa wapangaji wetu watapewa kipaumbele kupata sehemu ya makazi ndani ya nyumba hizo," alisema.

2 comments:

  1. hiyo nipoa hawa magabachori wamezidi kutuzid kete kila siku wanajenga apartment wanapangisha kwa bei za kufuru leo wanajifanya ni masikini wa hali za chini, hongera DG wa nhc na tafadhali mama Tibaijuka wasikuzid kete kwenye kikao

    ReplyDelete
  2. Hivi nyie mnaoomba kuuziwa hizi nyumba kwa hali yake ya sasa mbona mu wabinafsi kiasi hiki!!! taarifa imeshatolewa kwamba majumba hayo kutokana na kuchoka kupita kiasi yatabomolewa na kujengwa nyingine zitakazoweza kuchukua wapangaji wengi zaidi na hatimae kuuzwa kwa asilimia 70 ya nyumba hizo. Kwa kufanya hivyo wanunuzi watakuwa wengi kuliko mkiuziwa sasa. Msishinikize vitu vya ajabu mkumbuke hata sisitulio nje ya nyumba hizo tuna haki pia sawasawa na mliomo ndani ya nyumba.

    ReplyDelete