15 June 2011

Nidhamu bungeni yamkera Makinda

*Awafananisha wabunge na 'watu walioko Kariakoo'
*Kutoa ufafanuzi wa wabunge wala rushwa bungeni


Tumaini Makene na Pendo Mtibuche, Dodoma

TABIA ya baadhi ya wabunge kuzungumza bungeni bila kufuata taratibu wanapokuwa ndani ya ukumbi, imemkera Spika wa Bunge
Bi. Anne Makinda na kuamua kuwatolea uvivu, kwa kuwafananisha na 'watu walioko sokoni Kariakoo' ambako kila mmoja hujifanyia mambo yake kadri anavyoona.

Akizungumza huku akioneshwa kukerwa na tabia hiyo ya wabunge kuzungumza ovyo na kukosa usikivu wakati wenzao wanachangia hoja, kutofuata utaratibu wanapotaka kutoa taarifa au kuomba mwongozo, alisema 'alilazimika kuzima tv ili asiendelee kuwasikiliza'.

Spika Makinda aliyasema hayo jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu, akionesha jinsi ambavyo hakuridhishwa na namna wabunge walivyokuwa wakichangia hoja wakati wa kujadili Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Bw. Steven Wassira.

"Tunapokuwa hapa tunaangaliwa na wananchi, watu wanawaheshimu sana...sijui kwa nini ninyi mnakuwa hamjiheshimu, wanatushangaa tunavyozungumza bila kufuata utaratibu.

Jana (juzi) sikuwepo hapa bungeni wakati mkichangia mpango wa maendeleo, lakini nilikuwa naangalia kwenye tv mlivyokuwa mkichangia, yaani nilishindwa kuangalia kabisa, sikuwa na hamu ya kuangalia bunge, nikazima tv.

"Mtu anasimama wakati wowote kuomba mwongozo wa spika, mwingine anasimama anasimama naye anaomba mwongozo, mwongozo, mwongozo sasa inakuwa vurugu," alisema Spika Makinda na kuongeza.

Mwingine anaomba kuhusu utaratibu, mwingine anaye anasimama kutoa taarifa, kila mahali mtu anasimama anasema yake, huo si utaratibu, mnakuwa kama watu wa Kariakoo," alisema.

Aliwaonya wabunge kuwa iwapo wanataka kufanana na watu wa soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam watafanana, na iwapo hawataki pia watabaki ya heshima yao mbele ya jamii.

Hatua hiyo ilifikiwa na Spika wakati akitolea ufafanuzi wa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe baada ya kufuata taratibu za kuomba mwongozo wa spika, hali ambayo  spika huyo aliwataka wabunge wengine kuiga mfano huo.

Bi. Makinda alisema kuwa utaratibu alioutumia Bw. Mbowe wa kuomba Mwongozo kwa Spika ni mzuri, kwani alisubiri spika amalize kazi iliyowa mbele yake, na ndivyo alivyofanya
mbunge huyo mara baada ya kuona hajaridhika na majibu aliyopewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi.

Alisema kuwa hivi sasa wabunge wengi wamekuwa hawafuati taratibu za kuomba mwongozo ambapo kila mtu anasimama na kuomba mwongozo bila kujali hoja gani inaendelea mezani na kusema kuwa wabunge hao wanajidhalilisha kwa wananchi ambao wanawafuatilia
katika vyombo vya habari.

Akitoa mfano wa jinsi mbunge anavyotakiwa kuchangia hoja, kutoa dukuduku pale asiporidika na hoja au mchango wa mbunge mwenzake au majibu ya serikali, Spika Makinda alisema ni bora kwa kila mbunge kusoma na kufuata kanuni za bunge kuhusu majadiliano ndani ya bunge.

"Kama alivyofanya Mheshimiwa Mbowe sasa hivi ni sahihi alipoomba mwongozo wa spika baada ya kutoridhishwa na majibu ya waziri...yaani Mbowe yuko sahihi kabisa si kama mlivyokuwa mkifanya jana (juzi)," alisema Spika Makinda.

Alisema kama mtu hujaridhika na jibu alilopewa anatakiwa subiri taratibu zinakwisha unaomba mwongozo wa spika...kuhusu utaratibu na si kila mtu kusimama anapojikia kusema.

Hata hivyo baada ya kumaliza kutoa onyo kali kwa wabunge Spika Makinda aliwaomba wabunge na wananchi kutotafsiri vibaya kauli yake kuwa amewabeza watu wa Kariakoo.

Alisema soko la Kariakoo kama ilivyo kwa masoko mengine hakuna utaratibu maalumu wa watu kuzungumza wanapokuwa katika shughuli zao za kujitafutia mahitaji ya kila siku.

“Sikudhamiria kuwakashifu watu wa Karikaoo, lakini nilitaka kumaanisha kuwa, ukienda Kariakoo watu hawana utaratibu wa kuzungumza, kila mtu anazungumza mambo yake, huyu anasema hivi na huyu anasema hivi, lakini, hapa hapana...tuna utaratibu wa kuzungumza.

"Kama nitakuwa nimewaudhi watu wa Kariakoo samahani sana, sikumaanisha nia mbaya, bali kuwatofautisha watu wa sokoni na wabunge katika utaratibu wa kuzungumza," alisema kiongozi huyo wa bunge.

Katika kikao cha bunge juzi jioni wakati wabunge wakijadili Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12-2015/16) ukumbi ulitawaliwa na vurugu kwa kila mmoja kutofuata kanuni kwa kusimama na kuzungumza bila kufuata utaratibu.

Moja ya hoja iliyoibua 'sokomoko' katika kikao hicho ni ya Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulira, ambaye katika hali isiyotarajiwa aliwataja baadhi ya wabunge wenzake kwa majina, akisema kuwa kuna mtandao unaohusisha wabunge na mawaziri, wanaoomba rushwa kwa watendaji wa serikali.

Hali hiyo ya kutofuata taratibu, ilimweka katika wakati mgumu Mwenyekiti wa Bunge, Bw. George Simbachawene (Kibakwe, CCM), ambaye alilazimika mara kwa mara, kusimama na kuweka hali ya mambo sawa, kwa kutoa maelekezo kwa wabunge kufuata taratibu.

Masuala mengine yaliyozua malumbano ya hapa na pale, hivyo wabunge kuzungumza bila kufuata utaratibu ni pamoja na maandamano ya vyama vya siasa nchini, mpango wa
maendeleo kutajwa kuwa ni wa chama tawala, wakati wengine wakisema ni wa taifa, hauna chama, huku pia suala la rais kusaini rasimu hiyo kabla haijajadiliwa ikizua hoja iwapo alisaini kama rais ama menyekiti wa Tume ya Mipango, kiasi cha
kulishukuru bunge, kabla hata halijaujadili.

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge, Bi. Makinda ameahidi kulitolea ufafanuzi bungeni suala la tuhuma za rushwa ambalo lilitolewa juzi na Bw. Kafulira, akiwatuhumu baadhi ya wabunge kwa kula rushwa, kutoka kwa watendaji wa serikali, katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Akijibu swali la Majira lililotaka kujua ukweli kuwa suala hilo lina muda mrefu mezani kwake, tangu Mei 24, mwaka huu, ambapo taarifa zinasema kuwa Bw. Kafulira aliliwasilisha mezani kwake, akitaka hatua zichukuliwe, Spika Makinda alijibu kwa
kifupi "nitalitolea maelezo hapa bungeni." 

Katika tuhuma hizo, Bw. Kafulila, alimtaja Mbunge wa Mbozi Mashariki, Bw. Godfrey Zambi (CCM), kuwa ni miongoni mwa wabunge watatu ambao anao ushahidi kwa kuwafuma wakiomba rushwa kutoka kwa watendaji wa serikali katika moja ya halmashauri nchini.

Mbunge huyo hakupata nafasi ya kuendelea kutaja majina ya wabunge wengine (Majira linayo ya wabunge wengine wawili) baada ya muda wake kuzungumza kuisha, hali iliyomlazimu Mbunge wa Mhambwe, Bw. Felix Mkosamali kuomba mwongozo wa mwenyekiti
ili aruhusiwe kuendelea kuwataja wabunge waliosalia katika orodha hiyo ya wabunge walioomba rushwa.

Baadaye Bw. Zambi aliomba mwongozo, akimwomba Mwenyekiti Bw. Simbachawene, amtake Bw. Kafulila kuthibitisha kauli yake na kuwasilisha bungeni maelezo yenye usahihi, kuwa yeye ni mla rushwa, akisema kuwa kitendo hicho cha kutajwa hadharani kimedhalilisha na kumshushia hadhi yeye binafsi na chama chake CCM, mbele ya wananchi.

"Hii ni character assassination (udhalilishaji), Mheshimiwa Kafulila kanitaja kwa jina kuwa mimi ni mla rushwa, amenidhalilisha mimi mwenyewe na chama changu, amesema
alinikamata nikipokea rushwa, naomba akuandikie barua na viambatanisho...lakini mimi namwelewa Kafulila, alifukuzwa CHADEMA kwa sababu ya kusema sema wenzake, hii ni kwa
sababu tuna vijana wanaotaka kulipuka tu, naomba hatua zichukuliwe ukweli ujulikane katika suala hili," alisema Bw. Zambi.

2 comments:

  1. Sokoine's cousin: wabunge wetu hawana ADABU HATA!!
    MIAKA 5 itakwisha na wataendelea kuongea upumbavu kwa miaka yote mitano!!!

    watanzania wenzangu sijui kwa nini mnaumiza vihcwa vyenu....!! ukiona watoto wa nymba fulani wana tabia chafu (kukosa malezi ya kimaadili), ujue hata wazazi wao wapo hivyo, hivyo!!

    ReplyDelete
  2. mama makinda, ukiona hivyo no kwa kuwa hakuna haki ndani ya kikundi! hata nyumbani kwako kama kuna mtoto mmoja wa kike halafu wakiume wako 10 inabidi baba na mama wawe na busara kuzuia wingi wa vijana wa kiume haubinyi haki ya msichana mmoja. Mbaya zaidi kama baba na mama mara zote wataunga mkono hoja za vijana 10 hata kama hoja zao mbovu na kupuuza hoja ya msichana mmoja hata kama hoja hiyo ina manufaa kwa wanafamilia wote na majirani. Bila wazazi ndani ya jengo la bunge kusimamia kwa haki basi watoto watendelea kupashana, kutukanana na kuomba mlango wa nyumba ufungwe, taa zizimwe ili wazichape! Na majirani (wanafunzi wa UDOM) watataka nao waingie kusaidia mpambano! Ustaarabu anza kuuonyesha wewe kama mzazi! Ushauri huu umetolewa bila malipo!

    ReplyDelete