15 June 2011

Mnyika: DAWASCO itoe maelezo kero ya maji

Na Stella Aron

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika, amelitaka Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) kutoa maelezo kuhusu hatua walizozichukua
katika kushughulikia kero ya maji katika baadhi ya maeneo ya jimbo lake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari na Katibu Msaidizi katika ofisi ya mbunge huyo, Bw. Aziz Himbuka, mbunge huyo tayari ameiandikia barua kampuni hiyo kutaka maelezo.

Katika barua hiyo, Bw. Mnyika anataka kujua hatua ambazo wamezichukua katika kushughulikia kero ya maji.

"Naelewa kwamba utatuzi wa kero ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo jimbo la Ubungo unahitaji hatua za muda mrefu, hata hivyo, zipo hatua ambazo zingeweza kuchukuliwa kwa haraka kuhusu mapendekezo ya muda mfupi lakini DAWASCO imeshindwa kutoa majibu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Majira ilipomtafuta Mtendaji Mkuu wa DAWASCO Bw. Jackson Midala, kujua hatua walizofikia katika kushughulikia madai ya mbunge huyo alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwenye vyombo vya habari kwa kuwa utazua malumbano bila sababu.

"Tulishatoa maelezo tangu mwezi wa tatu kuhusu suala hilo, sitaki malumbano na viongozi," alisema Bw. Midala.

No comments:

Post a Comment