15 June 2011

Ujambazi muhimbili ni uzembe-Kamanda Kova

Na Stella Aron

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Bw. Suleman Kova, amesema tukio la ujambazi wa kutumia silaha uliotokea juzi asubuhi katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuuawa kwa mlinzi wa Kampuni ya Full Time Ltd, Bw. Juma Mgungu, pamoja na kuibwa kwa sh. milioni 12.7 ni la kizembe.

Ujambazi huo ulitokea juzi wakati fedha zikihamishwa kutoka kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) kwenda Idara ya Uhasibu kwa ajili ya kupelekwa benki, ulisababisha pia mtumishi wa maabara Bi. Sabina Masawe, aliyekuwa akipita karibu na eneo hilo kujeruhiwa kwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Kova alisema kitendo cha walinzi wa eneo hilo kukosa silaha ni uzembe na kwamba wangeweza kupambana na majambazi hayo.

"Kama mlinzi huyo angekuwa na silaha kwa namna moja ama nyingine angeweza kupambana na majambazi na huu ni uzembe wa walinzi," alisema Kamanda Kova.

Hata hivyo alisema waajiri wanatakiwa kuwa makini na kwamba kumekuwa na walinzi ambao wanafanya kazi bila silaha, jambo ambalo linaweza kuwasababishia madhara makubwa.

"Sitopenda kuzungumzia zaidi kuhusiana na tukio hilo lakini Jeshi la Polisi linafanya upelelezi ili kuwabaini wahusika," alisema.

Katika tukio hilo majambazi walivamia katika hospitali hiyo na kupora sh. milioni 12.7 zilizochangwa na wagonjwa tangu Jumapili.

Kwa mujibu wa ofisa habari wa hospitali hiyo, Bw. Aminiel Aligaesha, watu watatu ghafla wakitumia pikipiki walivamia gari lililokuwa na wahasibu wawili, Bi. Farida Kabanda na Bw. Seleman Msaki na mlizi ambaye baadaye aliuawa.

Katika purukushani hizo jambazi mmoja lilipora mfuko wenye fedha na kutoweka pamoja na wenzake, huku wakirusha risasi.

No comments:

Post a Comment