13 June 2011

Mjadala wa bajeti moto wiki hii

Na Tumaini Makene

BUNGE leo linatarajiwa kuanza kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali katika wiki ambayo inatarajiwa kuwa ya mikiki na makeke mengi, kutokana na
mijadala kutoka kwa wabunge.

Hatua hiyo inakuja baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kuwasilisha makadirio wa mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2011/2012, huku pia Mkurugenzi wa Tume ya Mipango, Dkt. Phillip Mpango akitoa semina kwa wabunge juu ya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za bunge , mjadala wa bajeti ya
serikali utakaochukua siku tano, utaanza Jumatano Juni 15, mwaka huu, baada ya siku za mbili za mjadala wa mpango wa maendeleo, utakaowasilishwa bungeni leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Bw. Steven Wassira.

Bajeti ya Serikali

Baada ya Jumamosi kutumiwa na wabunge kufanya vikao vya kamati za vyama  vya siasa kuwekana sawa, mjadala wa bajeti unatarajiwa kuwa mkali ukivuta wachangiaji wengi kutokana na mwendo wa siasa nchini katika siku za hivi karibuni, kufanyika bungeni na nje ya bunge.

Mjadala huo utaanza mara baada ya kusomwa kwa hotuba ya bajeti mbadala kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambayo baadhi ya mapendekezo yake yameibua mjadala ndani ya jamii.

Baadhi ya masuala ambayo yanatarajiwa kuufanya mjadala wa bajeti kuwa mkali, ni pamoja na suala la kuondolewa kwa 'posho za vikao' ambazo watumishi wa umma na wabunge hulipwa, pale wanapokaa kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.

Suala hilo sasa limezua mjadala mkubwa nchini na kujengwa dhana kuwa posho zinazopendekezwa kukatwa, ni zile zinazowahusu wabunge pekee, wakati wanaotoa mapendekezo hayo wanashauri kufumuliwa kwa mfumo mzima ulioruhusu watumishi wa serikali kulipwa posho za vikao katika majukumu yao ya kazi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, pendekezo lao hilo ambalo litakuwa moja ya mapendekezo aliyoyaita 'magumu kwa watumishi wengi wa umma kukubaliana nayo', litaokoa takribani sh. bilioni 900 kwa mwaka.

Suala hilo tayari limeanza kupata ukinzani hasa kutoka ndani ya wabunge wenyewe, wengi wao wakiwa wa chama tawala, ambao wamenukuliwa wakisema
hawako tayari kuziachia posho hizo, kwani ni utamaduni walioukuta, hivyo waliotoa pendekezo hilo, ndiyo wanapaswa kuwa wa kwanza kuzikataa.

Waziri Mkulo tayari ameonesha msimamo juu ya hilo, akisema kuwa atawategea wabunge wa CHADEMA kwa kuwaletea fomu maalumu ili wajaze, kama hawazihitaji fedha hizo za posho, huku Spika wa Bunge, Bi. Anna makinda akisema hata wakizikataa atawawekea kwenye akaunti zao.

Hoja nyingine ambayo inatarajiwa kuwaunganisha wabunge wengi bila kujali vyama, ni juu ya mapato yanayotokana na rasilimali madini kutumika katika kuongeza pato la taifa katia kuchangia maendeleo ya watu, hasa kwa kupitia kodi.

Katika hotuba ya bajeti wiki iliyopita bungeni, serikali imekwepa kwa mara nyingine kurekebisha sheria ili kuzuia mianya ya kutolipa au kukwepa kulipa kodi katika sekta hiyo ya madini. Hakuna mahali ambapo inaonekana namna gani serikali itaweza kupata mapato zaidi kutokana na madini, suala ambalo limeonekana kuwa hoja kwa watu mbalimbali, wakiwemo wabunge mara tu baada ya kusomwa kwa bajeti hiyo.

Kwa muda mrefu kampuni kubwa za madini zimekuwa zikisamehewa kodi mbalimbali, hali ambayo imesababisha nchi kukosa mapato kutoka katika sekta hiyo nyeti ambayo imeendelea kukua kila kukicha, huku katika soko la dunia ikiendelea kuwa imara, hata wakati wa mtikisiko wa uchumi duniani.

Mmoja wa wabunge ambayo Majira lilipata fursa ya kuzungumza nao, akisema si vyema kunukuliwa kwa kirefu kwani atazungumza wakati wa mjadala wenyewe, alisemakwa kifupi kuwa wanataka mabadiliko ya sheria ya madini ili kupata mapato zaidi.

Hoja nyingine katika bajeti ni juu ya dhamira ya serikali kupambana na ukali wa maisha unaowakabili Watanzania sasa hasa kutokana na kupanda kwa gharama za bei za vitu mbalimbali, ambapo kwa mujibu wa Bw. Mkulo moja ya mikakati ni kuhakikisha bei ya mafuta, hasa petroli, ambayo kupanda kwake kumesababishwa na vitu mbalimbali, inashuka.

No comments:

Post a Comment