*Polisi wanasa watatu
Na Mercy James, Njombe
WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoania hapa kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la utekaji mtoto na kumchinja kwa kumtenganisha kichwa na
kiwiliwili.
Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Livingstone Njombe Mkoani Iringa Doris Lutego (12) alichinjwa na watu wasiojulikana Juni 12 saa sita za usiku.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa Kamishna msaidizi wa Polisi Bw. Evarist Mangalla, alisema, watu hao walikamatwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya polisi na wananchi.
Alisema watu hao wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo kwa kutumia mavazi ya baibui na mawigi vichwani katika shule hiyo kisha kumteka mtoto Doros kisha kutoweka naye ambapo jitihada za kumpata hazikufanikiwa hadi maiti yake ilipokutwa katika Kitongoji cha Kambarage Wilayani humo juni 12 asubuhi.
Kamanda Mangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bw. Christopher Msigwa (25) mkazi wa mtaa huo ambaye ni fundi magari,Bw.James Mtulo (20) na Michael Msemwa (32) wakazi wa kitongoji cha Nzengerendete,mjini Njombe.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya watoto walioona tukio hilo kwa karibu walidai kwamba watu waliomteka mtoto huyo walikuwa na mavazi ya kike huku wakiwa wamevalia nywele za bandia (wigi) vichwani.
Walisema mwingine alikuwa amevalia baibui na kwamba walibaini mavazi hayo wakati wa kurupushani wakati wa kumtoa mtoto wa pili ambaye hata hivyo alinusurika.
Mazishi ya mtoto Doris Lutego yalifanyika juni 14 na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa shule, makanisa, elimu,na kamati ya ulinzi na usalama wilaya.
Mazishi hayo yalifanyika katika makaburi ya ikingula huku Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba, akitoa mwito kwa wamiliki wa shule za bweni kuimarisha ulinzi katika shule hizo pamoja na kuajiri walinzi waliopitia mafunzo wenye uwezo wa kukabiliana na wahalifu.
Alisema ili kukomesha vitendo hivyo ni lazima sheria ichukue mkondo wake kwa garama yoyote ile.
Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo waliwahi kuhusishwa katika tukio kama hilo ambalo lilitokea Januari 7 mwaka huu.
Katika tukio hilo mtoto mmoja alitekwa na watu wasiojulikana kisha kukutwa katika eneo hilo hilo akiwa ameng'olewa meno yote kinywani hali iliyosababisha watuhumiwa kudhani kuwa alikuwa amekufa badala yake alikuwa amezimia na kukimbizwa Hospitali ya Ikonda kwa matibabu
Katika hatua nyingine watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa licha ya kuhusishwa katika tukio la awali waliachiwa huru kabla ya kufiishwa mahakamani.
Kutokana na hali hiyo wananchi walijiuliza maswali mengi na kufuatilia kwa karibu tukio ambapo wengi wamelalamikia watuhumiwa kuachiwa huru huku vitendo hivyo vikiendelea.
Katika tukio jingine Bw. Daud Mkoveke (25) Mkazi wa Mbaramaziwa Wilaya ya Mufindi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumua kwa kumkata na Jembe kichwani Bw. Sales Mhume (60).
Tukio hilo lilitokea Juni 13 saa 11. 30 jioni katika Kijiji cha Mbaramaziwa, na kamba kiini cha mauaji hayo kinachunguzwa na watuhumiwa katika matukio hayo wanatarajia kufikishwa mahakamani baada ya uchuguzi kukamilika.
Matukio ya mauaji katika mkoa wa Iringa yamekuwa yakiongezeka kila kukicha hali inayosababisha hofu kwa wananchi.
Msemaji wa polisi Mkoa wa Iringa alisema kuachiwa kwa watuhumiwa mara kwa mara unatokana na usiri wa wananchi katika kufichua waovu kwa kuhofia visasi.
Alisema wananchi wanapotakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi zao wamekuwa hawafiki jambo ambalo linazidi kuwapa mwanya wahalifu kuendeleza matukio hayo wakiamini kuwa kesi zao zitafutwa.
Ahsante sana kwa habari ya Livingstone School
ReplyDeleteBig up sana mamaaa