14 June 2011

Majambazi waua, wapora mil. 12/- Muhimbili

Mfanyakazi wa Maabara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Bi.Sabina Massawe akiwa chumba cha Upasuaji cha Hospitali hiyo baada ya kupigwa risasi na majambazi waliopora fedha kiasi cha Sh.Mil 12.7 Dar es salaam Jana.Katika tukio hilo mlinzi wa Kampuni ya Full Times Security Bw.Juma Magungu aliuawa.

Na Aisha Kitupula

WATU watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevamia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana saa 2 asubuhi na na kuua askari mmoja kisha kupora
sh. milioni 12.7.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Hospitali ya Muhimbili, Bw. Aminiel Aligaesha alisema tukio hilo lilitokea wakati wahasibu wakihamisha fedha hizo kutoka Idara ya wagonjwa wa nje mahali zinapokusanyiwa kwenda Idara ya Uhasibu hospitalini kwa ajili ya maandalizi ya kwenda benki.

"Baada ya dereva kuegesha gari lenye namba SU 36713 aina ya Pick-Up lililokuwa likiendeshwa na Bw. Said Fungo ilitokea pikipiki ikiwa na watu watatu wakiwa na silaha na kuvamia gari lililokuwa na wahasibu wawili Bi. Farida Kabanda na Bw. Selemani Msaki pamoja askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Full Time, Bw. Juma Magungu na kurusha risasi huku wakitaka pesa ambazo ni mapato ya siku tatu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili," alisema Bw. Aligaesha.

Alisema kuwa majambazi hao walimpiga risasi askari upande wa kulia chini ya kwapa na askari huyo alifariki dunia muda mfupi baadaye, huku risasi nyingine ikimpata mfanyakazi wa baabara, Bi. Sabina Masawe mguuni na kutokea kiunoni. Bi Masawe alikuwa akipita bila kujua kinachoendelea.

Bw. Aligaesha aliongeza kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo walitoa taarifa polisi na walifika, lakini wajambazi hao walikuwa wameshaondoka eneo la tukio na uchunguzi zaidi unafanywa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo.

Naye Bw. Optatus Silanda ambaye ni Meneja wa Magojwa ya dharura Muhimbili alisema kuwa amepokea majeruhi wawili Bi. Masawe ambaye ni mtu wa maabara na Bi. Jackline ambaye alikwenda Hospitali kumuangalia ndugu yake ambaye alipata mshtuko na kudondoka.

Bw. Silanda alisema kuwa majeruhi hao na wanaendelea vizuri na wapo kwenye matibau kwenye kitengo cha magonjwa ya dharura.

Akizungumza na gazeti hili, Bi. Masawe alisema yeye alikuwa anapita njia ghafla akashtukia kuona mguu wake ukivuja damu, hivyo alioomba msaada na kupelekwa wodini na kudai kuwa anaendelea vizuri ila bado anasikia maumivu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Bw. Faustine Shilogile hakupatikana na simu yake iliita bila kupokelewa.

3 comments:

  1. wizi kama huu ni mipango tu,watu wanaelekezwa kila kitu,simu zinafanya kazi,nendeni ktk mitandao ya simu mutakuta mipango yote imesukwa vipi,hakuna kipya,hata kama simu hazipatikani tena lakini mesage zote ziko mitandaoni,kwa nini wasikamatwe,simu zipo,fanyeni kazi polisi.poleni sana wafiwa na majeruhi

    ReplyDelete
  2. Maskini, familia ya Bwana Juma, poleni sana na Mungu awatie nguvu.Huo wizi wa namna hiyo ni kweli ni njama. Anzeni na huyo mhasibu yawezekana kuna mpango uliochorwa. Siku hizi dunia ni kama kijiji hakuna siri tena.

    ReplyDelete
  3. Ni kweli ndugu Anonymous wa 10:45 PM kuwa simu zinafanya kazi. Lakini watu wananunua laini za simu, hawasajili namba na kwa hiyo hata zikifuatiliwa haitajulikana mawasiliano yalikuwa baina ya akina nani.

    Shinikizo la kusajili namba za simu lilikuwa la zima moto mno. Watu wananunua laini lakini hawasajili namba.

    ReplyDelete