14 June 2011

Kikwete asaini Mpango kabla ya kupitishwa

Na Tumaini Makene

MPANGO wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12-2015/16), umewasilishwa rasmi bungeni, huku wabunge wakianza kuuchambua, ambapo
imehojiwa sababu za Rais Jakaya Kikwete kuusaini, kisha kulishukuru bunge kwa kazi yake ya kuupitisha, kabla hata haujawasilishwa kwa ajili ya kujadiliwa na kuridhiwa na bunge.

Akiuwasilisha mswada huo mbele ya bunge jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Mahusiano na Uratibu Bw. Steven Wassira, alisema;

"Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 63(3)c, inaelekeza kuwa kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake, bunge laweza-kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo."

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse, akinukuu kifungu hicho hicho cha katiba, alisema;

"Mheshimiwa Spika kwanza kabisa napenda kuwasilisha masikitiko ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na  mpango huu...wakati katiba ikitamka hivyo, mpango huu tayari ulishasainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania tangu tarehe 7 Juni 2011 na kuwasilishwa bungeni tarehe 8 Juni, kama hati ya kuwasilisha mezani, bila kuelezwa ndani ya mpango wenyewe kama kilichowasilishwa ni rasimu.

"Aidha kwa mpango wenyewe, rais tayari ameshashukuru wadau kwa maoni yao
yaliyowezesha kukamilisha mpango na ameshalishukuru bunge kwa mchango katika
kukamilisha mpango husika. Mheshimiwa Spika wakati Rais anasema hivyo, Kambi ya Upinzani Bungeni haijawahi kushirikishwa wala kushiriki kikao chochote cha bunge kilichojadili na kupitisha mpango huu.

"Kwa hiyo Kambi ya Upinzani inamtaka waziri aeleze ni kikao kipi cha bunge na ni mkutano wa ngapi wa bunge, uliowahi kujadili na kupitisha mpango huu wa maendeleo na hata kumpelekea mheshimiwa rais kulishukuru bunge kupitia dibaji yake iliyochapwa kwenye kitabu cha mpango huu."

Mchungaji Natse alisema kuwa Kambi ya Upinzani inalitaka bunge kufanya kazi zake kikamilifu, huku akiitaka serikali kuuhesimu mhimili huo wa serikali, isiwe na utamaduni wa kuamini kuwa kila jambo litakalowasilishwa bungeni litapitishwa, hivyo akasema ni muhimu maoni yatakayotolewa na wabunge yaingizwe na yafanyiwe kazi.

Suala hilo la Rais Jakaya Kikwete kusaini rasmu ya mpango huo, kisha kulishukuru bunge, kabla hata haujaingia bungeni ulianza kuzua maswali tangu wakati wa semina ya wabunge na Tume ya Mipango, Ijumaa wiki iliyopita, ambapo mmoja wa wabunge alihoji kwa nini imekuwa hivyo na iwapo maoni yao yataingizwa katika kitu ambacho kinaonekana kuwa kimeshapitishwa.

Huku akipinga pia matumizi ya lugha ya kiingereza katika suala muhimu kama hilo kwa maendeleo ya taifa kwa miaka mitano ijayo, kwani hautaweza kufahamika kwa Watanzania takriban asilimia 80, Mchungaji Natse aliongeza pia kuwa ni ajabu mpango huo kutozingatia katiba mpya.

Mbali ya hayo, mapema Bw. Wassira aliliomba Bunge kupokea na kujadili mapendekezo ya mpango huo, ili kuridhia utekelezaji wake, kulidhia mapendekezo kuwa mwaka wa fedha 2011/12 uwe ni kipindi cha mpito katika utekelezaji wa mpango huo ili kutoa fursa  kwa mpango kuanza kutekelezwa kikamilifu kuanzia mwaka wa fedha 2012/13. Pia liridhie vipaumbele vya mpango huo na mapendekezo ya rasilimali zinazohitajika kuutekeleza.

"Maeneo ya kipaumbele na malengo ya utekelezaji kwa kipindi cha miaka mitano ni yafuatayo; miundombinu, hasa upatikanaji wa nishati ya umeme toshelevu na ya uhakika kwa mahitaji ya ndani na kuuza katika nchi jirani. Sanjari na hili, mkazo umewekwa katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, hasa bandari, reli na barabara kuiwezesha Tanzania kuwa lango kuu la kibiashara na huduma kwa nchi jirani zisizo na bahari.

"Malengo ya utekelezaji ni kuongeza uzalishaji wa umeme kufikia 2780 MW; kuboresha njia za usafirishaji umeme na usambazaji; kujenga barabara za lami zenye urefu wa km 5,205; kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo bandarini kufikia tani 9.87 milioni na usafiri wa anga kusafirisha tani 35,500," alisema Bw. Wassira.

7 comments:

  1. WAPINZANI NA WABUNGE WA CCM WANAWEZA KUPITIA NA KAMA KUNA KASORO WAREKEBISHE. RAIS SIO MUNGU NAYE ANAWEZA KUKOSEA. HIVYO TUSIWE WATU WA KULALAMIKA TU, BALI TUTOE MICHANGO ITAKAYOSAIDIA. NAAMINI SIYO KILA KILICHOMO HUMO NI KIBAYA.

    ReplyDelete
  2. Ndugu yangu matanzania mwenzangu sio kuwa kila kitu ni kibaya ila ni kosa na ukosefu wa akil pale mtu mzima unaposimama bungeni na kuanza kuusifi huo mpango, watukuwatuma kwenda pale kusifiana pale wameenda kuukosoa utawala kwa mambo ya blanda wanayo fanya

    Hivyo mtanzania mwenzangu nikuombe uweze kutafakari kwa kina jambo kabla hujazungumza. Sasa kama kila kitu kitakuwa kusifu na kupongeza tu kuna haja ni nini kwenda pale mjengoni na wakalipwa hizo posho wanazongangania zisifute. Kweli wabunge wetu wengi hawatambui hata pale wamefuata nini. Mungu wasamehe kwani 2015 sio mbali sana mm najipanga na niwe masikini lakini lazima tujitoe kutetea maslai ya taifa letu

    ReplyDelete
  3. rais amekosa dira kama nchi imemshinda iiache kwani anayoamua mengi hayana maslahi kwa wananchi Tanzania sio mali yake,kama amekosa busara aseme,itakuaje mpango ambao unajadiliwa na haujakamilika anasaini hivi anafikiri nchi inaendeshwa kama atakavyo,aache ujinga

    ReplyDelete
  4. Inaonesha dhahiri kwamba bunge halina fursa ya kubadili ama kurekebisha chochote kinachotoka serikalini. Mtu utawashukuruje watu kwa michango yao wakati hawajakupa mchango wowote? Kwa maoni yangu, hakuna haja ya kupoteza muda- waurudishe kwenye drawing board!
    Hata hivyo kuuita mpango wa miaka 5 halafu kiukweli ni miaka 4 tayari kuna waa. Kwanini usifanyiwe kazi, ukachambuliwa kwa kina ili kuweka kila kitu sawa, halafu ukaanza rasmi mwaka ujao? Kama suala ni miaka 5 ya urais, basi uwe mpango wa miaka 4, ijulikane kabisa kwamba hawakufanya kitu mwaka huu wanaoubatiza ni wa transition. (The truth is, mwaka huu hakitafanyika kitu - kwa mujibu wa bajeti ya Mkulo)

    ReplyDelete
  5. KILA SIKU MIPANGO MIPYA TUJIULIZE JE MKUKUTA NA ULE WA MILENIA UMEFIKIA WAPI?SIO KUIBUA MIPANGO KILA WAKATI INAPOONEKA SERIKALI IMEBANWA NA WANANCHI HUO MPANGO NI USANII WATUPE FEEDBACK YA MKURABITA NA MKUKUTA NA ZILE AHADI TAKRIBANI 65 WALIZOAHIDI KWENYE KAMPENI

    ReplyDelete
  6. Mtoka mbali lakini mjini nafika; mzee hapo kachemsha; hivi unaweza kuingia kwenye nyumba hata kwenye nyumba ya ndugu bila kupiga hodi na kukaribishwa! ukifanya hivyo wa2 watakuwa na mashaka na upeo wako wa kifikiri

    ReplyDelete
  7. Huo ni ubumbavu mtupu!!!it is ONLY in Africa where these things are possible...Guys it is time to be honest with each other and try to move our country forward by having a clear and honest debate...huu ushenzi wa kudanganyana iabidi huishe!!!!....Wabunge are very smart people I'm sure.....Wanaweza kufanya debate na kuamua maswala ambayo yanaweza kuwasaidia wazalendo...It is time to look at our consitution and significant changes are needed...Those 3 sectors (Excutive Branch-President and his people, Parliament & Judiciary need to be independent so we can checks & balances)....As it stand-outs now...Too much power to the Presidents office and that is WHY he can do what he is doing....We were lucky we had MWALIMU-very honest President, NOT today guys...AAMKENI WATANZANIA....It is good to have differences BUT we can't afford to be enemies.....BRAVO & MUNGU IBARIKI TANZANIA..

    ReplyDelete