20 June 2011

Jalada la ajali ya Jaji Lugazia kutua mahakamani

Na Rehema Mohamed

MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP) Bw. Eliezer Fereshi, amesema upelelezi wa tukio la ajali ya gari iliyokuwa ikiendeshwa Jaji Projestus Rugazia, umekamilika na
jalada la shauri hilo litafikishwa mahakamani wakati wowote.

Katika ajali hiyo iliyotokea jijini Dar es Salaam, Oktoba 3, mwaka jana mtu mmoja, Salehe Omary wa Msasani Dar es Salaam, alikufa na wengine watatu kujeruhiwa.

Bw. Fereshi alitoa kauli hiyo alipozungumza na gazeti hili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja yanapofanyika Maonesho ya Wiki ya  Utumishi wa Umma.

Bw. Fereshi alisema ofisi yake ilikuwa ikisubiri kukamilika kwa  upelelezi wa kina kuhusiana na tukio hilo kabla ya kufikishwa mahakamani.

Alisema jalada lake hiyo litafikishwa mahakamani siku yoyote kama inavyofanyika kwa wengine.

"Kulikuwa na upelelezi, sasa umeshakamilika na tutapeleka mahakamani jalada hilo," alisema Bw. Fereshi

Jaji Rugazia (56) mkazi wa Ada Estate Kinondoni Oktoba 3, mwaka jana alipata ajali iliyosababisa gari lake kugonga magari matatu, ambapo mtu mmoja alikufa na wengine wanne kujeruhiwa.

Waliojeruhiwa ni Issa Idd (30) mkazi wa Kinondoni, Nasibu Hassan (28), mkazi wa Kitunda na mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), aliyejulikana kwa jina moja la Rahma.

Jaji Rugazia ambaye naye aliumia katika ajali hiyo, alikuwa akiendesha gari namba T.780 ACB aina ya Toyota Land Cruiser Prado.

Magari aliyogongwa ni T.776 AZK Mitsubishi Pajero, T.213 AZR Toyota Spacio, T.104 BHY Daihatsu Teriors, T.395 AKU Toyota Corolla na T.312 ACB Suzuki Escudo.

1 comment:

  1. UPELELEZI UMECHUKUA MUDA MREFU.
    Najiuliza kwanini upelelezi wa shauri hili umechukuwa muda mrefu kiasi hiki? Najiuliza swali hili kwa kuwa nimeshashuhudia baadhi ya ajali kubwa za barabarani kupita hii na upelelezi wake haukuchukua muda mrefu kama huu.Sipendi kuingilia uhuru wa mahakama au kujadili shauri liloko mahakamani ila nadhani mheshimiwa huyu kwa wadhifa wake hakustahili kuendesha gari alistahili aendeshwe na dereva wake kwani anaye na analipwa na serikali.

    ReplyDelete