Na John Daniel
SERIKALI imetoa msaada wa tani 2,076 za chakula katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ili kuwanusuru wananchi na njaa iliyosababishwa na ukame pamoja na
ugonjwa wa migomba na mihogo.
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka alisema jana kuwa hivi sasa anasaka sh. milioni 300 ili kusafirisha chakula hicho kutoka Hifadhi ya Chakula Mkoa wa Shinyanga.
"Nashukuru sana serikali kwa kutoa tani 2,076 za chakula kutoka Shinyanga, wananchi wa Muleba tunahitaji malori kama 70 ya tani 30 kusafirisha chakula hadi Muleba.
Wazabuni wengi wanataka sh. 300 kwa kilomita moja, na umbali kutoka Shinyanga hadi Muleba ni kilomita 550, ndio maana nimejichimbia huku kabisa na viongozi wenzangu tupate hizo fedha," alisema Prof. Tibaijuka.
Alisema licha ya serikali kutoa chakula hicho cha msaada chenye tahamni ya sh. milioni 860 pia ilitoa sh. milioni 32 kwa ajili ya kusafirisha chakula hicho lakini bado hazijafikia hata robo ya mahitaji halisi ya sh. milioni 300.
"Mimi ni Mbunge wa Muleba Kusini lakini kama waziri lazima nishughulikie wilaya nzima ya Muleba yenye wananchi takriban 450,000. Japo yapo maeneo yaliyoathirika zaidi," alisema.
Alisema chanzo cha njaa hiyo ni kutokana na migomba kukumbwa na ugonjwa wa kunyauka, kuharibika kwa mazao ya mahindi pamoja na mihogo kushambuliwa na ugonjwa.
"Kwa wale wananchi wanaotegemea uvuvi nao wamekwama, ni wakati wa kufunga uvuvi kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana," alisema Prof. Tibaijuka na kuongeza.
"Mimi nilijifunza kutoka Umoja wa Mataifa, ukitaka kugawa chakula ni lazima mpango wa kugawa utangulie chakula, wakati tunatafuta pesa pia naweka utaratibu wa ugawaji ili kusije kukatokea vurugu na malalamiko.
Kama unavyojua Muleba ni mbali sana, iko pembezoni na huku vijijini usafiri ni tabu kidogo ni lazima uandae kila kitu mapema ili wale watakaopewa bure kabisa wajulikane pamoja na wale wataoachangia angalu sh. 100 tu kwa kilo," alisema.
Alisema tayari amefanya mawasiliano na Shirika la Kimataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ili kuona uwezekano wa kupata msaada zaidi wa usafiri.
Alisema Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika itawaandikia ili kuona kama wanaweza kusaidia kwa hatua yoyote. Kuhusu shule zilizoezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua alisema tayari serikali imetoa msaada wa sh. milioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa shule saba za msingi na sekondari mbili zilizoezuliwa.
Tunatoa shukurani kwa Serekali kwa kuwajali wannchi wa Muleba, Tuntoa rai, Serekali iongeze kiwango cha msaada kwa kugharimia usafiri ili chakula kiwafikie walengwa.
ReplyDeleteHapo muone uzuri wa kuwachagua viongozi walioelimika na wanaojari utu wa mtu. Sio wanaoingia bungeni kuganga njaa kama mwenzake wa Kasikazini
ReplyDelete