Na Benjamin Masese
CHAMA cha Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli ya Tanzania (TRL) kimeweka wazi msimamo wake kwa kusema kuwa endapo Serikali itatoa mabilioni yaliyotengwa kwa
ajili ya ukarabati wa reli,bila ya kuambatanisha fedha hizo na kifuta jasho chao, hazitafanya chochote na badala yake zitaishia mikononi mwao kwa kuwa wao ndio wasimamizi.
Mbali na hilo, kimesema kwamba msimamo wa kudai haki zao bado utaendelea kuwepo kwa kuwa chama kipo na mwajiri wao yupo huku kikisisitiza kwamba kufariki kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa TRAWU, Bw. Slyvester Rwegasira si kikomo cha kufuatiliwa kwa suala hilo.
Msimamo huo uliwekwa Dar es Salaam jana na Mwenyeti wa TRAWU Taifa Bw. Bakari Kiswala katika mkutano wa wafanyakazi uliokuwa na mada nne ikiwemo ya kudai kifuta jasho, taarifa ya kuvunjwa mkataba, kumwombea dua aliyekuwa katibu mkuu, marehemu Rwegasira na maandalizi ya kuziba nafasi hiyo pia kupinga kauli inayotolewa na Waziri wa Uchukuzi, Bw. Nundu kwa Rais Jakaya Kikwete iliyodai kuwa wafanyakazi wa TRL ni wakorofi na hawatawaliki.
Hata hivyo kabla ya Bw. Bakari kuhutubia wafanyakazi hao, walianza kwa kuomba dua zilizoambatana na nyimbo za maombolezo huku wakisisitiza kuendeleza mazuri aliyokuwa akiyafanya.
Bw. Bakari alisema kuwa kifo cha marehemu Rwegasira ni pengo kubwa kwa chama cha TRAWU hivyo kamati ya utendaji inatarajia kukaa hivi karibuni ili kuziba nafasi hiyo.
Alisema nafasi hiyo itashikwa na mtu mwenye msimamo mkali na kuwataka wafanyakazi kumpa ushirikiano na kutokuwa wanyonge kwa kuamini kuwa madai yao lazima yatekelezwe kwa kuwa mwajiri na chama bado vipo.
Bw. Bakari alisema kwa mujibu wa taarifa alizopata kutoka Wizara ya Uchukuzi juzi ni kwamba RITES ambaye ni mwekezaji wa TRL ataachia ngazi rasmi mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumzia kauli ya Bw. Nundu kuwa wafanyakazi wa TRL ni wakorofi na hawatawaliki, alisema kauli hiyo ni ya kutaka kuwachafua kwa Rais wao na wananchi kwa ujumla kwani sababu za ukorofi wao zilishindwa kufafanuliwa ndani ya kamati za bunge ilipokaa Machi 23, mwaka huu.
Hata hivyo walimtaka Bw. Nundu kuwaomba radhi kutokana na kuwaita mbele ya Rais ni wakorofi na hawatawaliki kabla yao kuonesha ukorofi wao.
Bw. Bakari alisema kwamba waziri wa uchukuzi mara atakaporudi kutoka bungeni Dodoma atakutana na safu nzima ya uongozi wa TRAWU ofisini kwake ili kuendeleza madai yao ya haki.
"Kama kifuta jasho hakitalipwa kwa wafanyakazi wa TRL hawatakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote na viongozi wa wizara hata kama serikali itaendelea kushikilia msimamo wa kutenga sh. bilioni 63 hazitabadili kitu chochote ndani ya kampuni hiyo licha ya mwekezaji kuondoka," alisema.
Kwa upande wa wafanyakazi waliitaka Menejimenti ya TRL kujivua gamba kama ilivyofanyika kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya Julai mwaka huu watakapoanza kuwaadhibu kwa vitendo.
Vile vile waliomba serikali kuwakamata walioingia mkataba mbovu na RITES na kuwafikisha katika vyombo vya sheria sambamba na kuwanyang'anya mali zao lakini pia wakaitaka serikali kusitisha mwekezaji kuendelea kupokea fedha zinazopatikana sasa.
No comments:
Post a Comment