11 March 2011

UEFA yawashitaki Wenger na Samir Nasri

BARCELONA, Hispania

KOCHA wa Klabu ya Arsenal, Arsene Wenger pamoja na mshambuliaji wa pembeni wa timu hiyo, Samir Nasri wameshtakiwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Ulaya (UEFA), kutokana na matamshi yao makali dhidi ya mwamuzi, baada ya kufungwa na Barcelona usiku wa Jumanne.

Msemaji wa UEFA, alisema shauri hili linahusu mwenendo mbaya wa kocha na mchezaji wake.

Alisema kwamba wanashtakiwa kwa kutumia "lugha mbaya" kwa mwamuzi, Massimo Busacca baada ya mpambano wa usiku wa kuwania ubingwa wa Ulaya, dhidi ya Barcelona.

Wenger alirushiana maneno makali na Busacca, baada ya kichapo cha mabao 3-1 kilichoitupa timu hiyo nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha Wenger alikasirishwa na uamuzi wa kutolewa nje mshambuliaji wake, Robin van Persie kwa kuoneshwa kadi ya manjano ya pili, wakati huo timu hizo mbili zilipokuwa nguvu sawa kwa kufungana 1-1, katika dakika ya 56.

UEFA imepitia ripoti ya mwamuzi Busacca, kabla ya kuwashtaki Wenger na Nasri.

1 comment:

  1. Wenger alionewa kwa kweli.Lakini haikumpasa kutumia lugha mbaya mchezoni

    ReplyDelete