11 March 2011

Jopo kuchunguza walioathirika mabomu Gongolamboto

Na Peter Mwenda

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Kitengo cha Magonjwa ya Akili imeunda kikosi kazi cha madaktari na wauguzi watakaopita nyumba 79 zilizoharibiwa
na mabomu Gongolamboto kutoa ushauri na kuwaondoa wasiwasi waathirika kuwaepusha kupata msongo wa mawazo.

Mratibu wa mpango huo, Bw. Cayus Mrina alisema kikosi hicho ambacho kilianza kazi jana kitapata nafasi ya kuzungumza na waathirika watakaogundulika kuwa wameathirika hivyo kupatiwa matibabu.

Alisema watu wengi walipata  matatizo ya kupata mshituko na kuathirika kisaikolojia baada ya kutokea milipuko ya mabomu katika makazi yao.

Alisema lengo jingine ni kuwarudisha waathirika katika hali ya kawaida kwa vile wengi wao wamepoteza ndugu, mali na viungo vya miili yao na kuwasababishia mawazo mengi.

"Watalaamu hawa wanatoka AMREF, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),Chama cha Madaktari cha Wanawake Tanzania (MEWATA),Manispaa ya Ilala,MUHAS na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)ambao tayari tumeanza kazi," alisema Bw.Mrina.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa MAT,Dkt.Kissah Mwambene alisema kazi ya kutoa ushauri huo kwa waathirika wa mabomu itakuwa bure.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa Mkoa Wa Dar es Salaam, Bw. Said Sadiki alisema idadi ya watu walikufa kwa mlipuko wa mabomu imefika 30.

Alisema idadi hiyo imeongezeka baada ya mgonjwa mmoja aliyekuwa amelazwa Muhimbili kufariki juzi na kuzikwa jana,Dar es Salaam.

Alisema majeruhi ambao bado wamelazwa hospitali hiyo kwa sasa ni 12 kati yao 8 wamelazwa Kitengo cha Mifupa (MOI) na wanne Muhimbili.

1 comment:

  1. ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema viongozi ndani ya Serikali, wamekuwa wakitenda mambo mengi mabaya dhidi ya wananchi na kuficha uozo wao kwa gharama yoyote.
    “Simameni daima katika ukweli; liwalo na liwe. Ukiogopa kufa leo utakufa kesho. Ukiogopa kusema ukweli leo eti ...kwa kuogopa kufa utakufa kesho,” aliasa watanzania Kadinali Pengo, kweli tumechoka tunataka mabadiliko.

    ReplyDelete