31 March 2011

Balozi Uholanzi atoa changamoto za kilimo

Na Tumaini Makene

WAKATI Serikali ya Tanzania ikieleza kuweka jitihada katika sekta ya kilimo kwa kuitengea bajeti kubwa, Balozi wa Uholanzi, Dkt. Ad Koekkoek, ameuliza maswali
'magumu' ikiwa ni changamoto kwa watafiti ili wachunguze kupata matokeo ya juhudi hizo kwa walengwa, ambao ni wakulima na nchi kwa ujumla.

Pia amebainisha kasoro kadhaa ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi na kuondolewa ili Tanzania iweze kufikia ndoto ya kuwa na uchumi unaomnufaisha kila Mtanzania, huku akisema kuwa mojawapo ni rushwa ambayo inasababishwa na udhibiti uliokithiri ukigubikwa na usiri mkubwa.

Akizungumza jana Dar es Salaam, katika kongamano la mwaka, kuadhimisha miaka 16 ya Taasisi ya Utafiti Kuhusu Kuondoa Umaskini (REPOA), Dkt. Koekkoek alisema kuwa wakulima nchini, ndiyo wajasiriamali wakubwa ambao kila Mtanzania anawategemea katika kukuza uchumi, kuongeza kipato na kutoa ajira.

"Ili kuongeza ajira unahitaji uongezekaji wa nafasi za kazi. Hapa Tanzania, nafasi hizo kwa kiasi kikubwa ziko katika sekta ya kilimo, pia katika utalii na pengine viwanda. Lakini kitu kimoja cha muhimu kujua ni kwamba kadri tija ya uzalishaji inavyozidi kuongezeka katika kilimo, watu wataondoka kutafuta kazi katika sekta
zingine.

"Sasa unafanikiwaje katika yote haya? Kwa miaka kadhaa sasa, serikali imekuwa na nia ya dhati na msukumo mahususi katika bajeti ya sekta ya kilimo. J,e hali hiyo imezaa matunda yaliyotarajiwa? Je, wakulima sasa wanazalisha zaidi? Je, sasa wanazalisha kwa tija? Je, kuna mkazo wowote katika kuwa na viwanda vya mazao ya kilimo?

"Haya ni maeneo muhimu kwa ajili ya utafiti na kufanyiwa mijadala. Je, serikali imetoa mchango wake kwa usahihi kadri inavyotakiwa? Je, imetoa msaada na kuwawezesha wakulima kama inavyotakiwa? Je, wakulima wana uhuru wa kuchagua kitu gani wazalishe, wanataka kuzalisha nini na kwa ajili ya nani?" alisema Balozi huyo wa Uholanzi hapa nchini.

No comments:

Post a Comment