14 February 2011

Wanachama 33 wa CCM wahamia CHADEMA

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga mjini kimepata pigo la aina yake baada
ya kukimbiwa na makada wake muhimu 33 waliokihama
chama hicho na kujiunga na Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo aliyekuwa mgombea wa kiti cha mtaa wa
Ndala.

Wanachama hao akiwemo, Bw. Juma Abdul aliyegombea kiti cha mtaa wa Ndala mwaka 2009
kwa tiketi ya CCM walirejesha kadi za CCM na kujiunga na CHADEMA juzi katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Ndala “A” Manispaa ya
Shinyanga ambapo pia wananchi walikula chakula cha pamoja na viongozi wa CHADEMA.

Bw. Abdul katika uchaguzi wa serikali za mtaa uliofanyika 2009 aliangushwa katika na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. George Sungura.

Mbali na Bw.Sunguraya kumwangusha mgombea wa CCM katika nafasi hiyo ya mwenyekiti wa mtaa pia katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka uliopita alimwangusha tena mgombea mwingine wa CCM, Bw. Gerald Tarimo katika kiti cha udiwani wa kata ya Ndala.

Mbali ya wana CCM hao 33 kuamua kukihama chama chao na kujiunga na CHADEMA pia wananchi wengine 42 walijiunga na CHADEMA akiwemo mmoja aliyerejesha kadi ya TLP baada ya kudai kufurahishwa na utendaji kazi wa madiwani wapya wa CHADEMA waliochaguliwa katika kata za Masekelo na Ndala Manispaa ya Shinyanga.

Hata hivyo katika hali iliyowashangaza wengi ni kitendo cha aliyekuwa mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM, Bw. Tarimo kuhudhuria katika mkutano huo ambapo alipewa nafasi ya kuwahutubia wananchi na kueleza  hakuwa na kinyongo chochote kutokana na ushindi alioupata mgombea wa CHADEMA na kwamba alishinda kihalali.

Bw. Tarimo aliwataka wakazi wa kata zote za Masekelo na Ndala kwamba mara baada ya
kukamilika kwa uchaguzi mkuu nchini hakuna haja tena ya kuendeleza malumbano ya kisiasa na badala yake wafanye kazi ambazo zitawezesha kusukuma mbele maendeleo yao na kwamba kwa kawaida siasa si ugomvi.

 Ndugu zangu siasa si ugomvi, kama kuna mtu anayefikiri kuwa siasa ni ugomvi huyo atakuwa anakosea, siasa si ugomvi, binafsi mimi nilikuwa mgombea kwa nafasi ya udiwani nikiwa na mwenzangu ambaye kura zake zilijaa, mheshimiwa  Sungura, bahati mbaya kura zangu hazikutosha, ni maamuzi ya wengi.

Jambo la pili ninalopenda kuwaeleza ndugu zangu mimi ni mwana harakati wa elimu hapa nchini, hivi sasa ninatengeneza kitabu kitakachoitwa Nauchukia ufisadi Tanzania’, kitakapokuwa tayari nitawapa viongozi wetu ili wawasambazie watu na waweze kuuchukia ufisadi kuanzia watoto wadogo wajenge tabia ya kumchukua mtu fisadi, alisema Bw. Tarimo.

Aliahidi kuchangia samani za ofisi ndogo ya CHADEMA katika kata ya Ndala ambapo hata hivyo aliwataka wana CCM wenzake wasimwelewe vibaya na kwamba alihudhuria katika mkutano huo baada ya kualikwa na viongozi wa CHADEMA kwa nia nzuri kwa vile siasa siyo ugomvi.

Kwa upande wao Bw. Sungura na Bw. Shelembi ambaye pia alikuwa mgombea ubunge kwa
tiketi ya CHADEMA katika Jimbo la Shinyanga mjini, waliwashukuru wananchi wote katika kata hizo kwa kuwachagua kuwa madiwani wao.

4 comments:

  1. Hapo kada wa ccm umenena na hongera maana ccm ilishapoteza mwelekeo ingawa wananchi wa shy tuna hasira kwa kuporwa ushindi wa ubunge wa shinyanga mjini ambao Mwanabiola shirembi MAGADULA alishinda kihalali lakini ccm Ilijitangazia ushindi kwa lazima!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Hakuna kitu bora kama hicho,chama kibakie na wenye imani na itikadi za chama,ni vyema wengi muondoke,wabakie wenye nia njema na chama. Pelekeni migogoro isiyoisha huko Chadema. CCM imekuwa na wanachama wa ajabu sana,akikataliwa/akishindwa kwenye kugombea nafasi yoyote ni nongwa,akipokonywa uongozi pia nongwa,ni bora ondokeni mkiache chama na wenye nia ya kukiongoza na kukitetea chama,chama ni sera na itatekelezwa na wanachama wenye nia ya dhati

    ReplyDelete
  3. NAWAPONGEZA WOTE MLIOCHUKUA UAMUZI HUO KWANI UKILA MCHICHA UKAONA ULE MCHICHA AUKULETEI AFYA SHARTI ULE NYAMA AU MAHARAGE HONGERENI KWA KUCHAGUA FUNGU JEMA

    ReplyDelete
  4. Wote hao ni watu wa maslahi tu wakishindwa sehemu moja wanakimbilia sehemu nyingine na wala sio kwa manufaa ya jamii ila kwa ajili ya matumbo yao na hiki chama cha CHADEMA pia sio cha kidemokrasia maan huyu mwenyekiti Mbowe anakifanya kama chake na jiulize kwa nini yeye asigombee uraisi kama mwenyekii na badala yake alimsukumia mwenzie?? anajua hana sera na hataki aibu anataka kukaa ktk kit milele na CHADEMA wapo walokua na uwezo wa kua mwenyekiti na kama atazidi kua mwenyekiti Mbowe basi wasahau kuchukua madaraka ya nchi muda wake wa uenyekiti pia umekwisha kama yeye ni mpena haki na anataka mabadiliko basi awape wengine nafasi asikifanye kamakiti cha urithi

    ReplyDelete