22 February 2011

Waliokufa Gongolamboto wafikia 26

Na Peter Mwenda

KATI ya majeruhi 512 wa ajali ya mlipuko wa mabomu uliotokea katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya 511 KJ, Gongolamboto
Dar es Salaam 59 ambao bado wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Amana na Temeke.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Judith Kahama akitoa taarifa za maafa ya mlipuko wa mabomu kwa Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama jana alisema kati ya majeruhi hao hospitali ya Muhimbili wamelazwa wagonjwa 36, Amana wagonjwa 20 na Temeke wagonjwa watatu.

Alisema milipuko hiyo iliyotokea Februari 16 ilisababisha vifo vya watu 26 na mpaka sasa maiti 24 zimechukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi na mbili zinasubiri kuchukuliwa.

Dkt. Kahama alisema siku ya tukio la kulipuka kwa mabomu jopo la madaktari wa mkoa wa Dar es Salaam waliomba msaada wa dharura kutoka hospitali kubwa jijini Dar es Salaam lakini walipata ushirikiano kutoka hospitali mbili za TMJ na Hindu Mandal.

Kauli hiyo iliamsha maswali kutoka kwa wabunge wa Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa wakitaka kujua kwa nini hospitali hizo zichukuliwe hatua kwa kushindwa kusaidia kutibu waathirika wa mabomu.

Mbunge wa Mji Mkongwe Zanzibar, Bw. Muhammad Sanya alisema hospitali hizo zimekosa uzalendo kwa kushindwa kujitolea kuokoa maisha ya waathirika wa mabomu ya Gongalamboto hivyo zitafutiwe adhabu.

"Mwenyekiti naomba kuuliza kwani hakuna sheria ya kuzibana hospitali ambazo zimeshindwa kutoa msaada wakati wa janga kama hili la Gongo la Mboto? alihoji Bw. Sanya.

Mwingine aliyechangia alikuwa Waziri wa zamani wa Afya, Bibi. Anna Abdallah aliyetaka kupata ufafanuzi namna ya kuzifanya hospitali binafsi kuchangia katika maafa.

"Wenye jukumu la kusimamia kupitishwa kwa sheria ya kuzibana hospitali binafsi ni kitengo cha maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu ambacho kinapaswa kupitisha muswada huo uende bungeni," alisema Ofisa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

No comments:

Post a Comment