22 February 2011

Mabomu yasababisha house girl apotezane na tajiri

Na Gladness Mboma

MSICHANA Ashura Shabani (17) mkazi wa Kigoma Ujiji amepotezana na tajiri wake Dar es Salaam baada ya kutokea milipuko ya mabomu iliyotokea
katika kambi ya 511KJ, Gongolamboto Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, msichana huyo ambaye amehifadhiwa katika kambi za Shirika la Msalaba Mwekundu zilizopo katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Ukonga alisema kuwa aliletwa jijini na mwanamke mmoja aliyemtaja kwa jina la Mama Mariam.

"Siku niliyofika Dar es Salaam nikitokea nyumbani Kigoma ndiyo siku ambayo ilitokea milipuko ya mabomu nikapotezana na tajiri yangu," alisema.

Alisema kuwa alikuwa ndani, mara mtoto wa tajiri yake aliyemtaja kwa jina moja la Mariam alimwambia atoke nje mama yake amekimbia kutokana na milipuko ya mabomu na kumtaka naye akimbie.

"Nilitoka nje nikaanza kukimbia, na Mariam sijui alikimbilia wapi nikajikuta nipo Magomeni Kituo cha Pplisi na watu wengine waliokimbia milipuko hiyo," alisema.

Alisema kuwa polisi waliwapeleka katika kambi hiyo na kwamba hawezi kujua nyumbani kwa tajiri yake kutokana na ugeni na kusisitiza kwamba angejua kama hayo yangemtokea asingekuja Dar es Salaam.

"Nimekuja kutafuta maisha ili niweze kumtunza mtoto wangu niliyemzaa nikiwa darasa la sita, lakini mabomu yamenirudisha nyuma," alisema msichana huyo kwa masikitiko huku akilia.

Msichana huyo alisema kuwa alipewa mimba na askari polisi mmoja (jina tunalo) ambaye alikataa mimba na mtoto lakini baadaye alifikishwa polisi akakubali kutoa huduma ya mtoto.

"Uwezi amini tangu nilipomzaa mtoto wangu Ismail, mzazi mwenzangu amenipatia sh.20,000 pekee na mtoto akiumwa ananiambia nipeleke vyeti ananunua dawa mwenyewe fedha hanipatii," alisema.

Alisema kuwa kutokana na mkasa huu uliompata hatamani tena kufanya kazi kwa mtu, hata kama tajiri yake atajitokeza kumchukua hatokubali tena kufanya kazi kwake kutokana na kutokuwa na imani naye.

Msichana huyo alisema kuwa kama tajiri yake huyo angekuwa anamjali angemtafuta siku ya pili yake ya mabomu na kwamba mpaka sasa hana mawasiliano yoyote na ndugu zake kutokana na kutokuwa na simu zao.

Alisema kuwa kuna ndugu zake wako Dar es Salaam, lakini hana mawasiliano nao kutokana na kutojua maeneo wanayoishi.

Msichana huyo alisema kuwa yeye ni mtoto wa mwisho wa familia hiyo yenye watoto watatu, ambapo baba yake alifariki mwaka jana na sasa amebaki na mama yake ambaye anamlelea mtoto wake huku dada zake wawili wakiwa wameolewa Rwanda na Mwanza.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadick alisema kuwa msichana huyo pamoja na wenzake watatu watasafirishwa kurudi kwao kama tajiri zao hawatajitokeza kuwachukua.

2 comments:

  1. WE MWANDISHI HABARI ZA POLISI KUZAA NAYE ZIMEKUJAJE? AU ANATAKUWA KAZETI LA IJUMAA? WE SEMA AMEPOTEA NA HUYO MAMA MARIAMU AJITAHIDI AAKAMCHUKUE , BASI. HAYO MENGINE NEXT TIME

    ReplyDelete
  2. Imekuwaje Polisi kuzaa na mwanafunzi na kuachiliwa kuendelea na kazi bila kufikishwa katika vyombo vya sheria. Je kweli hii ni haki Polisi kumwaribia mtoto elimu iliyo ufunguo wa maisha na kuachiliwa aendelee kufanya kazi aua aliyetoa habari hii ni uzushi basi. Tafadhali taarifa hii ichunguzwe ili ukweli ubainishwe na aliyefanya uhalifu huo (polisi)afungwe miaka 30 kama sheria inavyobainisha dhidi ya kosa kama hilo.

    ReplyDelete