LONDON, England
TIMU za Chelsea, Manchester United na Arsenal zimeendelea kufukuzana katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu wa England, baada ya kuibuka na
ushindi dhidi ya wapinzani wao katika michuano hiyo ya ligi.
Katika mechi hizo za usiku wa kuamkia jana, Chelsea iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Sunderland, Manchester United ikiwa kwenye Uwanja, Old Trafford ikailaza Aston Villa kwa mabao 3-1 huku Arsenal, ikitoka nyuma na kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Everton
Katika mchezo kati ya Chelsea na Sunderland, Nicolas Anelka alijibu mapigo ya ujio wa mchezaji mpya aliyesainishwa na klabu hiyo, Fernando Torres kwa kupachika bao moja na kutengeneza mengine yaliyoipa ushindi huo wa mabao 4-2.
Mshambulijai huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, ambaye namba yake ipo shakani kutokana na usajili uliovunja rekodi ya usajili nchini Uingereza, alipachika bao lake dakika za majeruhi na kuipa Chelsea ushindi wa tatu mfululizo kwenye michuano ya ligi.
Hata hivyo kabla ya bao hilo alikuwa ni kiungo wa Chelsea, Frank Lampard ambaye alisawazisha bao la dakika ya nne lililowekwa kimiani na Phil Bardsley kabla ya Salomon Kalou, kuifanya Blues iongoze dakika ya 23 baada ya kukimbia na mpira wa pasi aliyotengewa na Anelka.
Mchezaji Kieran Richardson ndiye aliyewasawazishia bao wenyeji hao dakika ya 26, lakini mabao waliyowekwa kimiani kipindi cha pili na wachezaji John Terry na Anelka, ndiyo yakaihakikishia Chelsea kuondoka na pointi za kutosha.
Matokeo hayo yanakifanya kikosi hicho cha Carlo Ancelotti, kubaki nyuma kwa pointi 10 dhidi ya vinara wa ligi hiyo ambao hadi sasa hawajafungwa, Manchester United.
Wakati Chelsea ikijitambia ushindi huo, Manchester United nao waliifunga Aston Villa mabao 3-1 katika Uwanja wao wa nyumbani Old Traford.
Katika mchezo Wayne Rooney alipachika mabao mawili kipindi cha kwanza na lingine likiwekwa kimiani na Nemenja Vidic kipindi cha pili na kuifanya timu yake kujikita kileleni ikiwa inaizidi Arsenal kwa pointi tano zaidi katika msimamo wa ligi.
Kwa upande wak Arsenal walifanikiwa kupata ushindi wao kwa mabao mawili ya kichwa yaliyofungwa na Laurent Koscielny, kipindi cha pili ndani ya dakika sita na kuifanya timu hiyo iweze kuondoka uwanjani na ushindi huo wa mabao 2-1 dhidi ya Everton.
Mshambuliaji wa Everton, Louis Saha ndiye alikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Arsenal dakika ya 24 kwa bao la utata lililopatikana baada ya Seamus Coleman, kupenyeza mpira kwenye ukuta wa Arsenal.
Hata hivyo bao hilo liliruhusiwa baada ya mpira huo kumfikia, Saha wakati mabeki wakijaribu kuokoa mpira huo.
No comments:
Post a Comment