07 December 2010

Taifa Queens uwanjani leo Singapore

Na Amina Athumani

TIMU ya taifa ya Tanzania ya netiboli 'Taifa Queens' leo saa 8 mchana itarusha karata yake ya kwanza katika michuano ya ufunguzi ya Kimataifa, inayofanyika nchini Singapore dhidi ya Scotland.Akizungumza kwa njia ya simu, Kaimu katibu Mkuu wa Chama cha
Netiboli Tanzania (CHANETA), Rose Mkisi alisema timu hiyo iliwasili juzi nchini Singapore, ikiwa salama na wachezaji wote wana morali ya kufanya vizuri.

Alisema timu hiyo pia itaingia uwanjani kesho, kuchuana na wenyeji wa michuano hiyo Singapore ambapo pia itachuana na India katika mchezo utakaofuata, kabla ya kumenyana na Namibia.

"Kwa kweli timu yetu ipo katika hali nzuri ya kiushindani na tunaimani itafanya vizuri, kutokana na maandalizi mazuri waliyopewa na Kocha Mkuu wa timu yetu, Simone Macknis," alisema Mkisi.

Timu hiyo iliondoka Ijumaa iliyopita ikiwa na jumla ya wachezaji 12, katika michuano hiyo itakayopandisha timu viwango vya kimataifa vinavyotambulika na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA).

Tanzania ni ya 22 kwa ubora wa viwango vya kimataifa, na kwa nchi za ukanda wa Afrika, Malawi ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Afrika Kusini huku Newsland ni ya kwanza kwa ubora duniani.

No comments:

Post a Comment