07 December 2010

Kuziona Kili Stars, Z'bar Heroes 1,000/-

Na Zahoro Mlanzi

MASHABIKI wa soka nchini watalazimika kulipa sh. 1,000 kiingilio cha chini na sh. 5,000 kiingilio cha juu kuzishuhudia timu zao za Tanzania bara 'Kilimanjaro Stars' na Zanzibar'Zanzibar Heroes' zitakapocheza robo fainali ya michuano ya Chalenji.Timu hizo
zitashuka uwanjani kesho kwa nyakati tofauti ambapo Zanzibar Heroes itakuwa ya kwanza itakapoumana na mabingwa watetezi Uganda 'The cranes' na Kili Stars itaoneshana kazi na Rwanda katika michezo itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni alisema baada ya kuona mashabiki wana moyo wa kuipa sapoti timu zao za Tanzania ndio maana wameamua kupunguza viingilio.

"Tumeamua kupunguza kabisa viingilio ambapo kwa viti vya kijani na bluu kiingilio kitakuwa sh. 1,000, viti vya mchungwa sh. 2,000, viti maalum C (VIP C) ni sh. 3,000, VIP B sh. 4,000 na VIP A sh. 5,000)", alisema Kayuni.

Alisema kati ya viti vyote vilivyopo VIP B, viti 400 vitatengwa kwa ajili ya waandishi wa habari, wachezaji ambao timu zao hazichezi, makamisaa na viongozi wengine, hivyo mashabiki watakaokaa eneo hilo wanaombwa kuwa watulivu zaidi.

Mbali na hilo, Kayuni alizungumzia pia michezo ya nusu fainali ambapo alisema itapigwa siku moja ya Ijumaa ambapo wa kwanza utaanza saa tisa na wa pili saa 11 na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utapigwa Jumamosi saa saba mchana ukifuatiwa na fainali.

Kayuni anawaomba mashabiki wa soka nchi kujitokeza kwa wingi katika michezo hiyo kwani muda waliowapa kudunbduliza fedha za kuingiliwa uwanjani hapo ni mwingi, hivyo wajitokeze kwa wingi.

No comments:

Post a Comment