23 December 2010

FRAT yaizulia jambo TFF

*Ni kuhusu beji za FIFA

Na Zahoro Mlanzi

SIKU moja baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutangaza waamuzi 14 kupewa beji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), imebainika miongoni mwao 'wamebebwa' kupewa beji hizo kutokana na
kujuana.

Kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), ambaye hakupenda kuandikwa gazetini kwa kuhofia kibarua chake, aliliambia gazeti hili Dar es Salaam jana kwamba miongoni mwa waamuzi hao, wanne kati yao hawakupitishwa na kamati yao katika majina yaliyokwenda FIFA.

Chanzo hicho kilisema kamati hiyo ya waamuzi ndiyo iliyopitisha majina yaliyotakiwa kwenda FIFA na si TFF kutumia ujanja kama walioutumia kupeleka majina tofauti.

Kilisema wanashangaa kuona majina waliyoyaondoa kuyakuta katika vyombo vya habari, yakitangazwa kwamba ndiyo yaliyopewa beji ya FIFA, kitu ambacho walishindwa kuelewa kimetoka wapi.

"Tunaomba waandishi mtusaidie katika hili, TFF wamechakachua majina tuliyoyapeleka kwao, nadhani kwa kuwa wao ndiyo watu wanaotakiwa kuyatuma FIFA, ndiyo maana wamefanya mchezo huo.

"Kuna waamuzi wanne ambao wana kashfa FIFA kwa kuchezesha mashindano ambayo shirikisho hilo hawayatambui, kila mwamuzi alihojiwa na FIFA kwa wakati wake na ikafikia hatua hata nchi ilitaka kufungiwa kutokana na hilo kwa kutoa kibali kwa waamuzi hao kuchezesha katika mashindano yaliyofanyika huko Al Qaeda," kilisema chanzo hicho.

Aliwataja waamuzi ambao waliachwa na FRAT ni Oden Mbaga, Hamis Chang'walu, Jesse Erasmo na mwingine kutoka Zanzibar na walioteuliwa na chama hicho ni Ferdinand Chacha, Alex Mahabi, Hashim Abdallah na Komba ambao walipitishwa na Kamati ya Waamuzi ya FRAT.

Kilisema viongozi wa juu wa FRAT wanalijua hilo, lakini wanashindwa kulianzisha kwa kuhofia vibarua vyao ila baada ya taarifa hizo wajumbe mbalimbali walipigiana simu kuonesha kushangazwa na majina yaliyotolewa.

Gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya waamuzi, Shaibu Nampunde kuzungumzia suala hilo, ambaye alikiri kwamba waamuzi hao kweli waliwekwa kando ili kusubiri hatma ya FIFA juu ya matatizo yao.

Alisema kwa kawaida hupeleka majina 10 ya waamuzi wa kati na 14 ya waamuzi wa akiba, hivyo kama FIFA imeamua kutumia majina ya akiba, badala ya yale waliyotakiwa kutumika, hajui ni vigezo gani vilivyotumika.

"Kweli hao waamuzi walikuwa na matatizo na FIFA na ndiyo maana sisi tukaamua tuwaweke kando ili wasubiri mpaka uchunguzi wa FIFA utakapokamilika, ila kwenye orodha ya majina iliyokwenda huko FIFA yalikuwepo, sasa sijui vigezo gani walivyotumia kuwapa ili hali hatujapewa taarifa zozote," alisema Nampunde kwa njia ya simu akiwa Nachingwea.

No comments:

Post a Comment