30 November 2010

Shinyanga wamzuia Shibuda awahutubie.

Na Suleiman Abeid, Shinyanga.

MBUNGE wa Maswa Magharibi mkoani Shinyanga, Bw. John Shibuda jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzuiwa na wananchi wa mjini Shinyanga wakishinikiza aongee
nao.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 asubuhi katika eneo la Machinjioni mjini Shinyanga wakati mbunge huyo alipokuwa amepeleka gari lake gereji kwa ajili ya
matengenezo madogo kabla ya kuendelea na safari yake ya wilayani Maswa.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wananchi hao kumfuata na kumzingira katika eneo la gereji iliyopo jirani na Machinjio ya Mji wa Shinyanga kwa lengo la kumjulia hali, ambapo ghafla kundi la vijana wengine liliongezeka na kumzuia asiondoke bila ya kuongea nao.

Wananchi hao walimuomba mbunge huyo awafafanulie mambo kadhaa ya kisiasa yakiwemo madai ya aliyekuwa mgombea wa CHADEMA katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Bw. Philipo Shelembi kupokwa ushindi.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya vijana hao walifuata jamvi na kulitandika kando ya barabara ambapo waliketi huku Bw. Shibuda akipewa kiti cha plastic pamoja na
kununuliwa soda aina ya Sprite ambapo walisema wakati anapokunywa soda hiyo awe akiwapatia ufafanuzi wa masuala waliyomuuliza.

Bw. Shibuda alilazimika kutii ombi la wananchi hao kwa kuanza kuwatoa wasiwasi wa kukamatwa na polisi kwa vile pale hapakuwa na mkutano wowote ulio rasmi na kwamba
kitendo walichokifanya ni sehemu ya haki yao ya kikatiba ya kukutana na wawakilishi wao wanaowachagua kuwawakilisha bungeni bila kizuizi chochote.

Kuhusu suala la mgombea ubunge katika jimbo la Shinyanga kupokwa ushindi wake, alisema tayari suala hilo limeanza kufanyiwa kazi ambapo viongozi wa chama hicho pamoja na mgombea tayari wamekwenda mahakama kuu mkoani Tabora kufungua rasmi kesi ya kupinga matokeo ya ubunge katika jimbo hilo.

Hata hivyo, alisema yeye kama mbunge wa CHADEMA atashirikiana na uongozi wa chama chake ili kuhakikisha haki ya wapiga kura katika jimbo la Shinyanga Mjini
inapatikana kwa kutangazwa mbunge halali aliyeshinda katika uchaguzi huo.

“Tumesikia kilio cha wananchi wa Jimbo la Shinyanga Mjini, ni kweli kuna uwezekano mkubwa wa Bw. Shelembi kuwa ndiye aliyeshinda, lakini zimefanyika hujuma na
msimamizi wa uchaguzi akamtangaza mgombea wa CCM, Bw. Steven Masele kuwa ndiye mshindi,” alisema.

“Lakini tunachosema ni kwamba ni vizuri sasa mahakama ikaamua kupitiwa upya kwa matokeo yote ya kila kituo ili iweze kufahamika mshindi halali alikuwa nani, na
tunaiomba serikali ihakikishe kesi itakapoanza, isikilizwe katika mahakama ya wazi ili kila mwananchi aweze kufuatilia maendeleo ya kesi hiyo,” alieleza Bw. Shibuda.

Bw. Shibuda aliwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati taratibu za kesi ya kupinga matokeo katika jimbo lao zikifanyika na kwamba wasiwe na wasiwasi wowote ule kwa vile mahakama nchini zipo kwa ajili ya kutenda haki.

3 comments:

  1. Je Chadema wamejipanga vipi kuhusu wasimamizi wa uchaguzi/wakurugenzi kubadilisha hata kura za masanduku za kila kituo na hivyo kupoteza ushahidi mahakamani??

    ReplyDelete
  2. Wananchi wanahamu ya kusikia toka kwa watu wao waliowaamini na kuwapa madaraka ya kwenda kutetea haki zao, wapeni nafasi msiwazuie kwani ni haki yao,asante jeshi la polisi kwa kulitambua hilo.

    ReplyDelete
  3. kwakweli wananchi tuna hamu sana ya kusikia kutoka kwa viongozi wetu, serikali itupe uhuru huo kwani ni haki yetu, hongera jeshi la polisi kwa kulitambua hilo.

    ReplyDelete