01 December 2010

Sherehe za Uhuru zaikwaza TFF

Na Mwandishi Wetu.

MECHI za awali za mashindano ya Kombe la Chalenji, zimeshindwa kupigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kama ilivyopangwa awali kutokana na maandalizi ya
sikukuu ya Uhuru wa Tanzania.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga alisema walipata maelekezo kutoka serikalini kwamba uwanja huo, utatumika kwenye sherehe za sikukuu ya Uhuru.

"Ni kweli tulipanga michezo ya awali ipigwe kwenye uwanja huo (Uhuru), lakini wenzetu wa serikalini wakatuambia tusiutumie kwa sasa mpaka watakapomaliza shughuli zao," alisema Tenga.

Alisema kutokana na hilo ndiyo maana wakaamua waombe michezo yote ifanyikie kwenye Uwanja wa Taifa, jijini licha ya uwanja huo kuendeshwa kwa gharama.

Akizungumzia kuhusu makato ya uwanja huo, alisema wanadhamini wameshamalizana na serikali kila kitu na endapo kama kutakuwa na madeni hakuna shaka watayabeba wao, kama wadhamini.

Akijibu kuhusu serikali kukiuka utaratibu waliojiwekea kwamba uwanja huo usitumike mara tatu kwa wiki, alisema hakukuwa na njia mbadala ndiyo maana wakaamua hivyo.

Alisema tayari mashindano hayo yalishatangazwa na timu zilishawasili, hivyo ingekuwa ngumu wasubiRi mpaka sherehe hizo za Uhuru zimalizike au kuahirisha mashindano.

No comments:

Post a Comment