26 November 2010

Inter, Barca, Man United zatinga 16 bora.

ROME, Italia

MABINGWA watetezi wa klabu bingwa Ulaya, Inter Milan usiku wa kuamkia jana walifuzu hatua ya mtoano baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya FC Twente  katika mechi iliyofanyika
katika uwanja wa San Siro.

Timu ya Rafael Benitez ililazimika kufanya kazi ya ziada kwa kucheza kwa kujituma kabla ya Esteban Cambiasso kufunga bao dakika 55 kwa mpira wa adhabu.

Barcelona ilipanda juu katika Kundi D baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya  Panathinaikos.

Pedro alifunga mabao mawili dakika za 27 na 69 kutokana na juhudi za Lionel Messi, ambaye alicheza kwa kiwango kizuri, naye alifunga bao dakika ya 62.

Barca imefikisha pointi 11 inafuatiwa na FC Copenhagen yenye pointi 7.

Wayne Rooney alicheza kwa mara ya kwanza tangu aliposaini mkataba mpya wa miaka mitano katika klabu ya Manchester United na kufunga bao pekee la ushindi dhidi ya Rangers katika uwanja wao na kuifanya mimba ya Old Traford kufuzu hatua ya 16 bora.

Rooney, alifunga bao dakika ya 87 na kupeleka sokoni kipa Allan McGregor baada ya united kupata penalti kufuatia Steven Naismith kumchezea faulo Fabio.

Valencia iliungana na United kusonga mbela katika Kundi C baada ya kuichabanga mabao 6-1 klabu ya Bursaspor katika uwanja wa Mestalla,mabao yao yalifungwa kipindi cha kwanza.

Juan Mata alifunga bao la kwanza kwa penatti na kisha
 Roberto Soldado, Aritz Aduriz  na Joaquin walifunga mabao mengine na kufanya timu yao kuongoza kwa mabao 4-0 hadi mapumziko.

Soldado  alifunga goli la tano baada ya Pablo Batalla kufunga goli moja kwa Bursaspor, mchezaji aliyetokea benchi Alejandro Dominguez alifunga bao la sita kwa Valencia.

United katika kundi lake ina pointi 10 ikiwa ni tatu zaidi ya Valencia. Katika mechi ya mwisho timu hizo zitacheza zenyewe.

Tottenham imeungana na Inter kusonga mbele katika kundi A, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Werder Bremen. Mabao yake yaliwekwa kimiani na Younes Kaboul  na Luka Modric.

Gareth Bale alikosa penalti kabla ya Peter Crouch kufunga bao la tatu, na kufanya Spurs kuwa ya kwanza ikiwa na pointi 10 sawa na Inter.

Timu ya FC Twente yenye pointi tano itacheza michuano ya Ligi ya Europa.

Timu nyingine zilizosonga mbele katika Kundi B ni Lyon ambayo msimu ulipita ilifika nusu fainali, licha ya kufungwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Schalke, ambayo pia aimesonga mbele.

Mabao mawili yaliyofungwa katika dakika 20 za kwanza na Jefferson Farfan na Klaas-Jan Huntelaar yalifanya timu hiyo ya ujerumani kutawala mchezo na kisha Hunterlaar alifunga bao la tatu.

Ushindi huo umefanya Schalke kufikisha pointi 10, ikiwa ni pointi moja zaidi dhidi ya Lyon.

Benfica ya Ureno ilichapwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Hapoel Tel Aviv. Waisrael walipata mabao yao kupitia kwa Eran Zahavi (mawili),  na jingine lilifungwa na Douglas da Silva.

Katika mechi nyingine ya Kundi D, Rubin Kazan ilifufua matumaini ya kucheza hatua ya mtoano ya timu 16 baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 ikiwa nyumbani dhidi ya FC Copenhagen .

Nahodha Cristian Noboa alifunga pao pekee na kuifanya Rubin kufikisha pointi sita, wanazidiwa pointi moja na wapinzani wao.

Timu nyingine zilizotangulia kufuzu hatua ya mtoano ni Buyern Munich katika Kundi E, ambayo inaweza kuungana na ama Roma au Basle. Kundi F Chelsea, Real Madrid na AC Milan Kundi G.

No comments:

Post a Comment