25 November 2010

BAE yakiri makosa kesi ya kashfa ya rada.

Na Tumaini Makene.

KAMPUNI ya Serikali ya Uingereza inayoshughulika na uuzaji wa zana za kijeshi (BAE Systems), imekiri makosa katika kesi ya kashfa uuzaji wa rada ya kijeshi kwa Serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian la Uingereza toleo la juzi, BAE, ambayo ni kampuni kubwa ya silaha imekiri kuwepo kwa matatizo ya hesabu, katika hatua ambayo ni mwendelezo wa kuhitimisha uchunguzi wa muda mrefu wa mazingira tata, yenye harufu ya rushwa.

Kwa mujibu wa mapendekezo yaliyofikiwa kati ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) na BAE Systems, kampuni hiyo imekiri kuwa kulikuwa na makosa katika mahesabu katika mkataba wake na Serikali ya Tanzania juu ya ununuzi wa rada hiyo.

BAE ilikiri mapungufu hayo juzi katika Mahakama ya Mji wa Westminster, London na sasa kesi hiyo itapelekwa katika Mahakama ya Juu ya Makosa ya Jinai, iitwayo 'Crown Court' kwa ajili ya hukumu Desemba 20.

Gazeti hilo liliripoti kuwa hata hivyo makubaliano hayo lazima yapitishwe na jaji wa mahakama ya juu zaidi inayoshughulikia jinai, iitwayo 'Crown Court' huku kukiwa na mijadala ya kisheria juu ya mamlaka iliyonayo SFO kuweka makubaliano na BAE katika hatua hiyo ya awali.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, makubaliano baina ya SFO na BAE yamekumbana na upinzani kutoka kwa wanaharakati wa vita dhidi ya rushwa wanaosema kampuni hiyo 'imesamehewa kirahisi sana.'

The Guardian limeripoti kuwa SFO ilitumia miaka mingi kuchunguza madai kuwa BAE ilitoa rushwa kwa baadhi ya wanasiasa na watendaji wa Serikali za Tanzania, Saudi Arabia, Romania, Afrika Kusini na Jamhuri ya Czech katika mikataba ya kuuziana zana za kijeshi.

Katika makubaliano ya awali kati ya BAE na SFO, kampuni hiyo ilisema iko tayari kulipa fidia ya Paundi za Uingereza Milioni 30 (Sh bilioni 72) kama adhabu ambapo kiasi fulani katika fedha hizo kitalipwa katika misingi ya wema, si kwa mujibu wa sheria, kwa Tanzania.

"BAE inatuhumiwa kuizuia Tanzania rada kwa mkataba wa paundi milioni 28 ambayo hata hivyo ilipingwa vikali na wataalamu kuwa iliongezwa bei na isiyokuwa ya muhimu kwa Tanzania, baada ya kutoa hongo inayokaribia robo tatu ya thamani ya rada hiyo.

"Kwa hivyo BAE, kupitia kwa David Perry, leo (juzi) wamekiri moja ya makosa kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni ya mwaka 1985 kwa 'kushindwa kutunza kumbukumbu za hesabu ambazo zingesaidia kuonesha na kueleza malipo' iliyolipa kwa kampuni mbili za Envers Trading na Merlin International, kati ya 1999 na 2005," lilisema The Guardian.

7 comments:

  1. Kwa maana hiyo Mr. Chenge ni beneficial ya hiyo hongo! na hakuna hatua yoyote dhidi yake so far! si haba hajaukwaa uwaziri hiyo ni hatua nzuri ya kumwandaa kwenda jela, sijui hukumu yake ya kuua kwa makusudi itaendaje! hofu yangu asijeleta immunity mbuzi hapa! wananchi wa Bariadi wajinga kwa kumpa kura zao, wawaulize wa kwa Mramba!

    ReplyDelete
  2. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 25, 2010 at 10:04 AM

    Haya Bwana Chenga,hapana Chenge mambo ndo hayo yanajiri..'stand still'!

    ReplyDelete
  3. Mhhhhh ama kweli Viongozi wetu Tanzania bado wamelala, kama Taasisi nyeti ya kupambana na rushwa ilimsafisha Mh. CHENGA, nadhani ni vema hata jina lake likabadilishwa sasa ili ifahamike kama ni TAASISI ya KUKUZA na KUINUA RUSHWA kwa sababu kama namba MOJA hajamuajibisha kiongozi wa TAKUKURU Watanzania tunatarajia nini?. Wakamatwe wapokea rushwa za Sh. ELFU KUMI TU. wa MABILIONI hizo sio rushwa ni VIJIZAWADI vya kuchezea WATOTO!

    ReplyDelete
  4. Hakuna jipya Tanzania,kama CCM ndiyo inayotawala basi msitegemee kuona hatua inachukuliwa kwa wala rushwa. Kuna mambo mengi yamezikwa kichini chini kama vile issue ya account ya malipo ya nje, ununuzi wa majenereta, na ubadhilifu wa pesa benki kuu. Wananchi wa Tanzania ndio wa kulaumiwa kwa kuweka CCM madarakani na kutofanya wawajibike.

    ReplyDelete
  5. haya chenge..sema sasa, mie siyo mwanasheria kama wewe ila nafahamu hata kama hautaswa cha muhimu ni kuwa umechafuka na unanuka mzee, na historia itakuhukumu tu na hata moyo wako unakuambia kuwa umechafuka ila kiburi tu

    ReplyDelete
  6. Chenge ni mzee wa changudoa!NendaLeaders Club utapata habari zake. Hata siku ya ajali alikuwa anatoka kwenye mission hizo hizo! Halafu nyie ndugu zetu wasukuma mna tatizo, kweli Chenge anafaa kuwaongoza!

    ReplyDelete
  7. Hata kama kampuni ya Uingereza imekubali kama ilitoa hongo kwa biashara zake na nchi nyingi zilizonunua vifaa toka kwake, bado hawana (hawatatoa )kumbukumbu walimhonga nani.Chenge hatatajwa kama alipokea pesa zao.Tanzania haina kesi na Chenge. Haina ushahidi!!Mkataba ulikuwa kati ya Tanzania na hiyo kampuni na siyo Chenge na Kampuni!

    ReplyDelete